Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, amefunguliwa mashtaka baada ya askari Polisi kumuweka kizuizini Mwalimu Hemed Said Masoud na nyumba yake kubomolewa kwa tuhuma za kujenga nyumba katika eneo la Jeshi la Polisi huko Limbani Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mwalimu huyo alikamatwa na kuwekwa rumande kabla ya kulazimishwa kuvunja nyumba hiyo akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, Novemba 22 mwaka 2005 akiwa nyumbani kwake katika mtaa wa Kizimbani, Pemba.
Katika kesi hiyo ya madai, Mwema anashitakiwa pamoja na viongozi watatu wa Jeshi hilo akiwemo Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Wete.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Usalama wa Raia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambao wote kwa pamoja wanatakiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 150 kutokana na kumdhalilisha mwalimu huyo na hasara iliyopatikana.
Kwa mujibu wa hati ya madai, mdai huyo anadai kuwa alikamatwa nyumbani kwake majira ya saa 5:00 asubuhi na kupelekwa katika kituo cha Wete kutokana na tuhuma za kuvamia uwanja wa Polisi na kujenga nyumba wakati eneo hilo akiwa amepewa na Idara ya Ardhi na Upimaji Zanzibar.
Anadai kuwa Polisi walimdhalilisha kumfunga pingu na kumuweka kizuizini kabla ya kumlazimisha kuvunja nyumba aliyokuwa akiendelea kujenga wakati yeye ni mmiliki halali wa eneo hilo.
Aidha, anadai kuwa baada ya kufikishwa Polisi alielezwa kuwa amefanya kosa la kupora kiwanja cha Polisi na kupewa masharti iwapo anataka kuachiwa huru akubali nyumba anayojenga kuivunja mara moja.
Mwalimu huyo anadai kuwa eneo la ardhi iliyokuwa ikijengwa nyumba ni mali ya urithi ya marehemu kaka yake marehemu Rashid Said Masoud, ambaye alipewa hati miliki ya ardhi ya Novemba 7 mwaka 1991 yenye kumbukmbu namba 65/5KAM/MK/974 na Idara ya Ardhi na Upimaji kisiwani humo.
Alieleza kwamba baada ya kulazimishwa aliamua kwenda kuvunja nyumba hiyo akiwa chini ya ulinzi wa askari wasiopungua saba ambao nao walishiriki kuvunja nyumba hiyo na ndipo baadaye akaachiwa huru baada ya kumaliza kuvunja nyumba hiyo.
Anadai kitendo hicho kimemzalilisha, kumvuruga kisaikolojia na kumrudisha nyuma kimaisha na kiuchumi na kumsababishia hasara ya Sh. milioni 35 kama gharama za ujenzi wa nyumba iliyokuwa imevunjwa.
Ameiomba mahakama iwalazimishe washtakiwa hao kulipa fidia ya Sh. milioni 70 kutokana na kitendo cha kuvunja nyumba bila ya sababu yoyote na kulipa Sh. milioni 15 kama fidia kutokana na kitendo cha kumzalilisha kwa kumfunga pingu na kumuweka kizuizini.
Vile vile aliiomba mahakama iwalazimishe wadaiwa wote kulipa Sh. milioni 30 kutokana na kitendo cha usumbufu cha kumlazimisha kuvunja nyumba yake akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari na Sh. milioni 35 wamlipe kama fidia ya uvamizi na maudhi wanayoendelea kumfanyia katika kiwanja chake namba 70, alichorithi kutoka kwa marehemu kaka yake, Rashid Said Masoud.