Watu wanne wamekufa papo hapo na wengine 37 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Songea kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka katika kijiji cha Lutukila Songea Vijijini mkoani Ruvuma.kwa habari zaidi....
Habari zilizopatikana mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamuhanda zilisema kuwa ajali hilo imetokea jana majira ya saa 1 asubuhi katika barabara ya Songea-Njombe iliyohusisha gari namba T 579 BDQ mali ya kampuni ya Superfeo ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Dereva Joseph Msigwa (48).
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Isaca Mhelela (13), mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Makambako mkoani Iringa, Hilda Ngombe (48), mkazi wa Bombambili mjini Songea , Elimina Ruben (2) na Regina Hamis ambaye alikuwa bado amefunikwa chini ya basi.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa Ruvuma, Dk. Benedikto Ngaiza, amethibitisha kupokea majeruhi 37 ambapo kati yao watatu hali zao ni mbaya na wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Aliwataja wagonjwa hao kuwa ni Sia Mtuhi (19) Feis Mtuhi wote wakazi wa Bombambili Songea, pamoja na dereva wa basi hilo Joseph Msigwa (42), ambaye amekatika mkono wa upande wa kulia na majeruhi wengine hali zao zinaendelea vizuri huku baadhi wakitibiwa na kuruhusiwa kurejea makwao.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo Aman Mmasi (38), alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi hilo ambaye alikuwa akikimbizana na basi jingine la kampuni hiyo na kushindwa kuhimili kukata kona na kupinduka kisha kugonga mti.
Kamanda huyo alisema wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa chanzo cha ajali hiyo na upelelezi ukikamilika wahusika watafikishwa mahakamani.
Hali hiyo ya ajali imesababisha mji wa Songea kukumbwa na wingu la huzuni kufuatia umati mkubwa wa watu kufurika katika Hospitali ya mkoa wa Songea kuwaona majeruhi na kuwatambua ndugu zao ambao walikuwa wanasafiri na basi hilo.