Boris Johnson amefuta ahadi ya malazi ya bure katika hoteli ya kifahari ya Dorchester mjini London kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya Fifa wakati wa michezo ya Olympic mwaka 2012.
Meya huyo wa London alitoa ahadi ya kuishi bure kwa Rais wa Fifa, Sepp Blatter pamoja na wajumbe wake.kwa habari zaidi..

Lakini uamuzi wa Fifa siku ya Alhamisi walipopiga kura ya nchi gani itakayoandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 - ambapo England ilikosa nafasi hiyo, ahadi hiyo imefutwa.
Urusi ilichaguliwa kuandaa mashindano hayo.
Vyumba vya bure vya kulala wageni mashuhuri ama VIP, vilitolewa na Locog, ambayo ni kamati ya maandalizi ya michezo ya Olympic.
Bw Johnson inaaminika alijadili suala hilo na mwenyekiti wa Locog, Sebastian Coe.
Meya huyo wa London hajaeleza chochote kutokana na uamuzi huo wa kufuta makazi ya bure kwa wajumbe wa Fifa.
Lakini baada ya kushindwa kwa England kupata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018, Bw Johnson aliyesafiri hadi Zurich binafsi kuwashawishi wajumbe wa kamati ya utendaji ya Fifa ili England ipatiwe nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia, alisema matokeo yalikuwa ni "pigo kubwa na wamekatishwa tamaa kwa kiasi kikubwa".