Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, Sambwee Shitambala, ambaye alitangaza kujiuzulu ili kupisha uchunguzi baada ya kutuhumiwa kuwa alihongwa Sh.milioni 400 na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kusababisha Chadema kushindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge jimbo la Mbeya Vijijini, amerejea katika wadhifa huo.
Alijiuzulu Novemba 22, mwaka huu kutokana na tuhuma hizo na hivyo kusabaisha wananchi kukosa imani naye.
Akitangaza kurejea katika wadhifa wake juzi wakati wa kikao cha Baraza la Ushauri la mkoa kilichohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbroad Slaa, Shitambala alisema amekubali kurejea baada ya kuridhika na uchunguzi uliofanywa na viongozi wa makao makuu kuhusu tuhuma zilizotolewa dhidi yake.
“Namshukuru Katibu Mkuu kwa kazi nzito aliyoifanya ya uchunguzi na kimsingi nimeridhika na uchunguzi wa chama kuhusu tuhuma za rushwa ambazo zilizagaa kila kona ya mkoa wa Mbeya na makao makuu ya chama na hivyo sasa baada ya kubainika kuwa sikuhongwa natangaza tena kurejea wadhifa wangu wa Mwenyekiti wa Chadema mkoa,” alisema Shitambala.
Alisema kiongozi yeyote makini unapokuwa unawaongoza wananchi lazima wajenge imani na wewe unapopata kashfa uwe mwepesi wa kujiuzulu na kwamba yeye anapenda sana mfumo wa vyama vingi viendelee kuwepo nchini kwa ajili ya kuleta changamoto kwa chama tawala.
“Tatizo katika nchi yetu watu au viongozi hawana tabia ya kujiuzulu hata wanapopata kashifa ukilinganisha na wenzetu wa Kenya, lakini mimi kama Shitambala sioni haya kujiuzulu, nataka hata viongozi ndani ya serikali na ndani ya Chadema wajenge tabia ya kujiuzulu wanapochafuka na wakisafishika wanarejea na madaraka kama kawaida,” alisema Shitamba.
Kwa upande wake, Dk. Slaa alisema chama kinampokea Shitambala kwa mikono miwili kwani tuhuma zilizokuwa zikitolewa dhidi yake hazikuwa za kweli bali zililenga kukivuruga chama.