Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amewataka wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya hifadhi za barabara, vinginevyo watashughulikiwa kisheria bila kujali jina la cheo cha mtu.
Magufuli aliyasema hayo juzi jioni mkoani hapa, alipotembelea maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Arusha–Namanga.
Alisema serikali imeweka wazi kuhusu umbali wa hifadhi za barabara, ambao ni mita 30 kutoka katikati ya barabara, hivyo akawataka wanaoendelea kujenga kwenye maeneo hayo kutambua kuwa sheria itachukua mkondo wake bila kujali cheo cha mhusika.
Alimwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Arusha, Deusdetus Kakoko, kuendelea kubomoa maeneo yote, ambayo yamejengwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara.
Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Arusha-Namanga, ambao umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa Sh. bilioni nane, alimwagiza mkandarasi wa ujenzi huo, kampuni ya China Geo Engeneering, kuhakikisha mradi huo unakamilika kama ilivyopangwa Julai 14, mwakani.
Alisema kuna baadhi ya vipengele vya mkataba kati ya serikali na mkandarasi huyo, ambavyo amevikiuka, likiwamo suala la kutumia magari chakavu wakati mkataba ulimtaka atumie mapya.
Alisema makandarasi wengi nchini, wamekuwa na desturi ya kuchelewesha miradi kwa makusudi na wengine kuwa na miradi mingi kwa wakati mmoja, hivyo kushindwa kuikamilisha kwa wakati na matokeo yake kuidai fidia serikali kwa kuwachelewesha wakati siyo kweli.