Goli lililofungwa kwa penati katika dakika ya 62 na nahodha Shadrack Nsajigwa’Fuso’ lilitosha kuipeleka nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ baada ya kushinda 1-0 katika mechi yao ya robo fainali dhidi ya Rwanda ‘Amavubi’ kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Habari zaidi...
Nsajigwa alifunga penati hiyo kwa ufundi katika uwanja ulionyeshewa mvua kipindi cha pili, akimpeleka kulia kipa wa Rwanda, Jean Luc Ndayishimiye huku mpira ukitinga wavuni upande wa kushoto. Penati hiyo ilitolewa na refa baada ya beki Eric Gasana wa Rwanda kumkwatua katika eneo la 18 mshambuliaji John Bocco.
Kabla ya hapo, Stars waliokuwa wakishangiliwa na maelfu ya mashabiki waliojazana uwanjani kabla ya saa 8:00 mchana, walikosa goli jingine la pili katika dakika ya 70 wakati shuti kali la Bocco lilipopanguliwa kwa ustadi mkubwa na kipa Ndayishimiye.
Baada ya ushindi huo, kocha wa Stars, Mdenmark Jean Poulsen, alisema amefurahishwa na wachezaji wake waliokuwa wakijituma katika muda wote wa mechi na kuongeza kuwa kazi haijaisha, na sasa wanajiandaa kwa mechi kali ya nusu fainali watakayocheza Ijumaa dhidi ya Uganda
Kocha Sellas Tetteh wa Rwanda aliwapongeza vijana wake kwa juhudi waliyoonyesha, lakini akamlaumu mwamuzi kwa kudai kuwa penati aliyowapa wenyeji haikustahili.
Awali, katika robo fainali nyingine iliyochezwa kuanzia saa 8:00 jana, mabingwa watetezi, Uganda waliendelea vyema na kampeni zao za kuwania ubingwa wa tatu mfululizo baada ya kushinda kwa penati 5-3 dhidi ya Zanzibar Heroes.
Licha ya kufungwa, Zanzibar walipambana kiume ambapo katika dakika 90 za kawaida, timu hizo zilitoka sare ya 2-2 kutokana na magoli ya Mike Sserugamba na la penati la Emmanuel Okwi (Uganda) na Zanzibar wakipata magoli yao kupitia kwa Khamis Mcha na Aggrey Morris.
Wakati wa ‘matuta’, Uganda walifunga penati zao zote zilizopigwa na Isinde Isaac, Sadam Juma Ibrahim, Godfrey Walusimbi, Tonny Maweje na winga Okwi wa klabu ya ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba. Penati za Zanzibar zilifungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro, Waziri Omar na Abdulhalim Humoud huku Morris akikosa penati ya utangulizi iliyopanguliwa na kipa Robert Odongkara.
Mechi za nusu fainali zitachezwa Ijumaa ambapo mbali na Stars kuwavaa Uganda, Ethiopia watacheza dhidi ya Ivory Coast na fainali itachezwa Jumapili.
Kikosi cha Stars: Juma Kaseja, Nsajigwa, Idrissa Rajab, Stephano mwasika, Kelvin Yondan, Juma Nyoso, Shaabn Nditi, Henry Joseph/John Bocco (dk.48), Mohamed Banka/Jabir Aziz (dk.17), Mrisho Ngassa na Nurdin Bakari.