Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi, kufuatia kifo cha ghafla cha mtoto wake, Dk. Suleiman Aboud Jumbe Mwinyi.
Dk. Suleiman Aboud Jumbe Mwinyi, mtoto wa kwanza wa Alhaj Jumbe, alifariki dunia Novemba 29, mwaka huu katika hoteli ya MDS Lodge iliyoko Sarita Vihar mjini New Delhi, India, ambako alikuwa amempeleka baba yake kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Apollo.
Kwa mujibu wa habari kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini India, Dk. Suleiman Jumbe Mwinyi, alikutwa na mauti chumbani mwa hoteli alimokuwa amefikia, na mwili wake ulitarajiwa kuwasili Zanzibar jana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia (ET) tayari kwa mazishi.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Alhaj Jumbe: “Nashindwa kuelezea kiasi cha majonzi na huzuni niliyopata baada ya kutaarifiwa kuhusu kifo cha ghafla cha mwanao, Dk. Suleiman Aboud Jumbe Mwinyi, na msiba huo mkubwa uliokufika."
Aliongeza: “Napenda kutuma rambirambi za dhati ya moyo wangu kwako kufuatia msiba huu mkubwa. Napenda kukuthibitishia kuwa mimi na wenzangu katika serikali tuko nawe katika msimba huu na katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi makubwa sana.”
Alimuomba Alhaj Jumbe kupitia kwako awasilishe salamu zake za rambirambi na wenzake katika Serikali kwa familia yake yote na kwa jamaa na marafiki ambao kwa namna moja ama nyingine wameguswa na msiba huu."
”Tunajua kuwa mnapitia kipindi kigumu. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awapeni nguvu, subira na uvumilivu wa kubeba majonzi ya kipindi hiki kwa sababu yote ni mapenzi yake.”