Aliyekuwa kiungo wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba, Haruna Moshi 'Boban' amekuwa katika wakati mgumu wa kusaka tiketi ya ndege ya kumpeleka Sweden kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Syrianska inayoshiriki ligi ya juu zaidi ya soka nchini humo.
Akizungumza jana, mmoja wa marafiki wa Boban, alisema kuwa licha ya Boban kusaka tiketi, pia amekuwa akishughulikia uwezekano wa kumalizana na klabu yake ya zamani ya Gelfe IF inayotaka ilipwe gharama zake kiasi cha dola 50,000 za Marekani kabla ya kumuachia aende kuchezea timu nyingine baada ya kukatisha mkataba wake wa awali.
Chanzo hicho kilisema kuwa klabu ya Syrianska imemueleza kiungo huyo kwamba itampokea wakati wowote atakapofika huko, lakini haikuwa na makubaliano ya kumtumia tiketi.
"Angekuwa na wakala ingekuwa rahisi kwa sababu angemsaidia gharama za tiketi na maandalizi mengine… lakini hivi sasa anashughulikia tiketi na kivyake na akienda huko, mambo mengi ya kulipa fidia kwa timu yake ya zamani yatazungumzwa," alisema rafiki huyo wa Boban.
Alisema kuwa Boban alifikia maamuzi ya kurejea Sweden baada ya kuona kwamba klabu za hapa nchini ikiwemo Simba, zimeshindwa kulipa gharama kubwa za kuvunja mkataba wake na Gefle IF.
"Simba hawakuwa wabishi baada ya kufahamu kuwa wao ndio waliopokea fedha hizo wakati wakimuuza, kwa hiyo ni lazima na wao wangelazimika kuzilipa fedha hizo endapo wangetaka kumrejesha," kiliongeza chanzo hicho.
Boban hakupatikana katika simu yake ya mkononi jana kuelezea ukweli kuhusu hatma yake na maandalizi ya safari hiyo ya kurejea Sweden.