Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, kuanzisha Siku ya Mtanzania kuadhimisha mambo mbalimbali ya kijamii katika ngazi ya Wilaya hadi ya Taifa ili kuuenzi utamaduni wa taifa.
Waziri Mkuu alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa sherehe za miaka 10 ya Siku ya Mtanzania ya Chakula iliyoandaliwa na Hoteli ya Peacock ya jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Karimjee.kwa maelezo zaidi
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu, kwa vyombo vya habari jana, ilimkariri Waziri Mkuu akisema kwamba kuna haja ya kuiadhimisha Siku ya Mtanzania kiwilaya, kimkoa na kitaifa na kupanua maudhui yake ili kuhusisha masuala mengine ya kijamii na burudani kama vile mavazi, ngoma, utawala na harusi.
“Bwana Mfugale (Joseph, Mkurugenzi Mkuu wa Peacock) amebuni Siku ya Mtanzania ya Chakula… Natoa wito kwa Watanzania wengine kufuata nyayo na ningependa wenzagu Serikalini wafikirie namna ya kufanya Siku ya Mtanzania kitaifa katika maeneo haya yote,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sherehe hizo zilihusisha vyakula vya asili kwa kanda za mikoa mbalimbali nchini, burudani ukiwemo muziki wa asili, wa dansi na sarakasi.
Miongoni mwa viongozi walishiriki ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Emmanuel Nchimbi na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na baadhi ya Wabunge.
Siku ya Mtanzania ya Chakula hufanywa na Hoteli ya Peacock kila Jumatano kwa kuandaa na kuuza vyakula vya asili vinavyopikwa kwa kutumia vyombo na majengo ya kisasa na wataalamu waliosomea mapishi, tangu mwaka 2000.