Mvua kubwa zilizonyesha jijini Dar es Salaam na mjini Songea, mkoani Ruvuma, usiku wa kuamkia jana na juzi, zimesababisha balaa kubwa zikiwemo vurugu na wananchi kupoteza makazi.
Mkanganyiko mkubwa jana uliwakumba abiria waliotumia Barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam, baada ya wakazi wa eneo la Tabata-Relini, kuweka vizuizi katikati ya barabara hiyo na kusababisha huduma ya usafiri wa daladala pamoja na magari ya watu binafsi kusimama kwa zaidi ya saa tatu.
habari na picha zaidi gonga hapo chini....
Barabara hiyo ilifungwa kuanzia saa 12.00 alfajiri hadi saa 3.15 asubuhi, baada ya wakazi hao kuweka vizuizi mbalimbali katikati ya barabara hiyo, yakiwemo mawe makubwa na madogo pamoja na magurudumu ya gari na hivyo kusababisha magari kushindwa kupita.
Hali hiyo ilizua tafrani na adha kubwa, baada ya usafiri wa daladala pamoja na magari ya watu binafsi yaliyotaka kupita katika barabara hiyo kukwama.
Kutokana na hali hiyo, watu wengi, hususan wafanyakazi, wafanyabiashara pamoja na wanafunzi, walilazimika kuchelewa kufika katika maeneo yao ya kazi na shuleni katika muda unaotakiwa kutokana na magari kukwama njiani.
Hali hiyo ilisababisha pia msongamano mkubwa wa magari yanayotumia barabara hiyo, na hivyo kuyalazimu baadhi ya magari kubadili njia na mengine kurudi yalikotoka.
Kadhalika, abiria wengi walilazimika kutembea kwa miguu na wengine kuingia gharama kukodi pikipiki ili kuwahi katika maeneo waliyokusudia kwenda.
NIPASHE ilifika katika eneo hilo na kushuhudia vizuizi hivyo vikiwa barabarani, huku msururu mrefu wa magari katika njia tofauti yaliyotaka kutumia barabara hiyo, yakiwa yamesimama kutokana na kushindwa kuendelea na safari.
Pia ilishuhudia mamia ya wakazi wa eneo hilo waliochachamaa pamoja na wapita njia waliovutiwa na tukio hilo, wakiwamo abiria waliokuwa ndani ya magari, wakiwa wamefurika katika eneo hilo kushuhudia hatma ya kilichokuwa kimetokea.
Wananchi hao walifunga barabara hiyo wakishinikiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuondoa mafuriko ya maji yaliyozingira nyumba zao na mengine kuingia ndani ya nyumba hizo na kuwasababishia hasara kubwa ya mali zao.
Baadhi ya hasara zinazodaiwa kusababishwa na mafuriko hayo, ni pamoja na uharibifu mkubwa wa vyakula, upotevu wa fedha taslimu na nyaraka mbalimbali.
Pia wakazi wengi, wakiwamo watoto wachanga, wazee na wagonjwa, kulazimika kulala nje kutokana na nyumba zao kujaa maji.
Wakazi hao wanadai kuwa walianza kukumbwa na mafuriko hayo kutokana na kalavati lililoko kandokando ya barabara hiyo kupitisha maji kidogo baada ya kujengwa chini ya viwango.
Hali hiyo inadaiwa kuwa imekuwa ikisababisha maji mengine yanayotoka katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Segerea, kukosa njia ya kupita na hivyo kutawanyika na kwenda kwenye majumba yao.
Kalavati hilo linalodaiwa kujengwa tangu mwaka 1985, linadaiwa kuwa sehemu ya mradi wa ujenzi unaoendelea katika barabara hiyo.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Maringa Seif, maarufu kama “Pua ya Ng’ombe” alisema mafuriko hayo yamekuwa kero ya muda mrefu na kwa hiyo jana waliona kwamba, iwe mwisho wake.
Hata hivyo, alidai kabla ya kuchukua hatua hiyo, mara kadhaa huko nyuma, wamekuwa wakilazimika kuingia gharama kutumia mashine ya kunyonya maji yanayofurika katika makazi yao.
Alidai wamekuwa wakifanya hivyo, huku wakipeleka malalamiko kwa maandishi kwenye mamlaka zinazohusika kulalamikia kero hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mandela, Omari Barua, lakini mara zote kilio chao kimepuuzwa.
“Sasa baada ya mvua ya jana (juzi) usiku kunyesha, tulimfuata mwenyekiti kumueleza kuhusu mafuriko ya maji kuingia majumbani, lakini akaonekana kulegalega kutokana na kukatishwa tamaa na wahusika, hivyo leo (jana) ndio tukaona tufunge barabara ili dunia ituonee huruma,” alisema Maringa.
Kutokana na barabara hiyo kufungwa, mmoja wa askari wa Kikosi cha Polisi wa Usalama Barabarani, alikwenda katika eneo hilo na kuwasihi wananchi hao kuondoa vizuizi hivyo barabarani.
Hata hivyo, askari huyo, ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, alikumbana na upinzani mkali na hivyo kutimka, baada ya wananchi hao kumjia juu na kutaka kumshambulia.
Dakika chache baadaye, askari polisi wa kawaida, pamoja na wa kikosi hicho na askari kanzu kadhaa, wakiongozwa na viongozi wao, walifika katika eneo hilo.
Kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Omari Barua, walianza kuwatuliza wananchi hao kwa kuwaahidi kwamba, wanayachukua malalamiko yao na kuyapeleka kwenye mamlaka inayohusika (Tanroads) ili kushughulikiwa mara moja.
“Serikali imepata taarifa na bosi wao huyu hapa (anamuonyesha mmoja wa viongozi wa polisi) amekuja. Ombi langu tufungue barabara. Tunakwenda kushughulikia na nitakuja na jibu kamili,” alisema Barua alipokuwa akizungumza na mamia ya wakazi hao waliofurika katika eneo hilo.
Hata hivyo, wakazi hao walichachamaa na kupaza sauti: “Hatutakiii!” hali ambayo iliwafanya viongozi hao wa polisi pamoja na Mwenyekiti huyo wa Serikali ya Mtaa kufanya kazi ya ziada kuwatuliza.
Mvutano huo ulidumu kwa dakika kadhaa, hadi aliposimama mmoja wa wakazi hao, Maringa na kutoa sharti kwamba, iwapo kero hiyo haitashughulikiwa ndani ya saa 24 kuanzia muda huo jana, wataendelea na msimamo wao wa kufungua barabara hiyo.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wakazi hao, ambao walimshangilia mwenzao huyo na kisha kwa pamoja, walishirikiana na askari polisi kuondoa vizuizi hivyo, kabla ya gari la kunyanyua vitu vizito kufika eneo hilo kuongeza nguvu na magari kuendelea na safari zake.
 Nyumba 236 zabomolewa Songea
Wakati huo huo, nyumba 236 zimebomolewa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kufuatia mvua ilionyesha juzi jioni katika maeneo mbali mbali ya mkoani humo kwa muda wa saa moja.
Mvua hizo pia zimewaathiri watu 196 kwa kuwaacha bila makazi
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Thomas Ole Sabaya, alisema kuwa nyumba hizo ziliezuliwa na kubomoka na kuziacha baadhi ya familia bila makazi.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa mitaa iliyoathiriwa zaidi na mvua hiyo ni Bombambili, Mfaranyaki, Misufini, Mjini, Mjimwema, Majengo, Ruvuma Lizaboni na Msamala ambapo pia madarasa 16 ya shule za msingi na sekondari yaliezuliwa na mengine kubomoka kutokana na mvua hiyo.
Sabaya alisema kuwa majengo ya utawala ya shule za msingi na sekondari ya Mfaranyaki na vyoo vitatu vya shule hiyo vimeezuliwa na kubomoka. Majengo mengine yaliyoezueliwa na kubomoka ni pamoja na ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata za Lizaboni na Matarawe.
Aidha, Sabaya alisema kuwa athari nyingine ni kuezuliwa kwa nyumba mbili za askari polisi zilizokuwa zikikaliwa na familia sita, ofisi ya Ofisa Elimu wa Manispaa ya Songea, ofisi za Kikosi cha Zimamoto pamoja na vibanda 12 vya biashara.
Sabaya alitoa pole kwa wananchi waliokumbwa na mkasa huo na kuwaomba wananchi wengine kuwasaidia walioathirika wakati serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari.

Imeandikwa na Muhibu Said (Dar) na Nathan Mtega (Songea).