Wanawake katika vijiji 40 mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro wamesema watawawajibisha viongozi ambao watashindwa kutekeleza ahadi za maendeleo walizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huu.
Wanawake hao wamesema walizisikia ahadi za wagombea kupitia mikutano ya hadhara na radio zinazotumia nishati ya jua au betri zilizotolewa na UNIFEM.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, UNIFEM ilitoa radio 400 aina ya Dynamo ambazo ziligawiwa kwa wanawake kwenye maboma ya Wamasai katika maeneo kadhaa ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Monduli na Longido mkoani Arusha na Same mkoani Kilimanjaro
Radio hizo zilitolewa ili kuwezesha jamii zilizoko pembezoni hasa wanawake kuweza kupata habari za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu na masuala ya maendeleo kwa ujumla.
Baadhi ya wanawake wa Kimasai walionufaika na radio hizo wamesema taarifa wanazozipata kupitia radio zinawatoa gizani kwani tofauti na miaka iliyopita mwaka huu waliweza kufuatilia habari za uchaguzi na habari nyingine nyingi kupitia radio hizo.
Wanawake kadhaa wa Kimasai huko Terrat mkoani Manyara, Oltepesy -Longido na Mti Mmoja Monduli mkoni Arusha wameiambia TAMWA mwishoni mwa wiki kuwa kupitia radio zao wanafuatilia pia masuala mbali mbali ya nchi hivi sasa.
“Hata Baraza la Mawaziri aliloteua Rais tumelisikia,” alisema Elena Kalembu kutoka Oltepesy, huko Longodo.
Vijiji vilivyonufaika na radio hizo ni Terrat, Orkaria, Loiborsiret, Lemkuta A, Naberera, Loiborsoit, Lemkuta B, Ormanie, Loondelemati A, Loondelemati B, Shuleni, Sabasaba, Mlimani, Ngarashi, Lendikinya, Madukani B, Emboreet, Madukani A na Lorng`oswani.