Mahakama Kuu ya Tanzania, imemwonya mfanyabiashara Yusuf Manji kuacha mara moja tabia ya kuchelewesha usikilizaji wa kesi inayomkabili mahakamani hapo kwa kutumia ujanja wa kubadilisha mawakili wapya kila inapopangwa kuanza kusikilizwa.
Onyo hilo lilitolewa na Jaji John Utamwa wakati akitoa uamuzi huo katika kesi ya madai namba 91 ya mwaka 2006 iliyofunguliwa mahakamani hapo na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited, Reginald Mengi, dhidi ya Manji.
Jaji Utamwa alitoa uamuzi huo kufuatia pingamizi lililowekwa na wakili wa Mengi, Michael Ngalo, baada ya kulalamikia ucheleweshwaji wa kesi hiyo.
Ngalo alidai kuwa ucheleweshwaji wa kesi hiyo umekuwa ukifanywa kwa makusudi na Manji kwa kupeleka mawakili wapya kila kesi hiyo inapokuja mahakamani kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Utamwa alisema mara ya mwisho kesi hiyo iliahirishwa Desemba 13 baada ya Manji kupeleka mawakili wapya.
Alisema mawakili hao wa Manji waliomba muda wa kupitia kesi hiyo kabla ya kuanza kuitetea.
“Desemba 13 kulikuwa na mawakili wapya, wakaomba tuahirishe ili wapate muda wa kuipitia. Leo wamekuja mawakili wengine wapya, nao wanaomba kesi iahirishwe ili wapate muda wa kuipitia,” alisema Jaji Utamwa.
Aliongeza: “Nakubaliana na Ngalo kuwa utaratibu wa kubadilisha mawakili kila kesi hiyo inapokuja, unachelewesha kesi na kuanzia sasa sikutakubali hali hiyo ijitokeze tena.”
Tangu kesi hiyo ilipowasilishwa mahakamani, baadhi ya mawakili waliojitokeza kumtetea Manji na baadaye kujitoa, ni Rathansi, Theonist Rutashoborwa, Muganyizi, Jamal na baadaye alirejea tena Rathansi.
Wengine ni Yuda Tadey, Dk. Ringo Tenga, Mabere Marando, Richard Rweyongeza, Tausi Abdallah na Cuthbert Tenga.
Baada ya kutoa uamuzi huo, mawakili wa Manji, ambao jana waliongozwa na Marando, waliingia katika mvutano mkubwa na wakili Ngalo, baada ya kuibua hoja ya kutaka washauri wa mahakama ambao ni Ndimara Tegambwage, Lugano Mbwina na Rose Haji wajitoe kusikiliza kesi hiyo.
Hoja hiyo ya kuwakataa washauri hao wa mahakama, iliibuliwa mahakamani hapo na Marando na kusababisha kesi ya msingi kusimama kwa takriban dakika 40.
Marando alidai anataka washauri hao wa mahakama wajitoe kwa madai kuwa ni wanahabari, hivyo wanaweza kuwa na mawasiliano na Mengi kwa vile ni mmiliki wa vyombo vya habari na pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (Moat). Wakili Ngalo alisimama na kuieleza mahakama kuwa haoni kuwa hoja ya upande wa utetezi kuwa ni ya msingi kwa vile washauri hao wako kisheria na walikuwapo tangu mwanzoni mwa kesi hiyo.
Ngalo aliongeza kuwa hata wasipokuwapo washauri hao wa mahakama, hawataathiri mwenendo wa kesi hiyo.
Katika uamuzi wake, Jaji Utamwa alitupilia mbali madai ya mawakili wa Manji na kuamua washauri hao wa mahakama waendelee kuwapo katika kesi hiyo na kusema sababu za uamuzi wake huo atazitoa baadaye.
Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Utamwa aliamuru kesi hiyo ianze kusikilizwa na shahidi wa kwanza kupanda kizimbani na kutoa ushahidi wake mahakamani hapo jana alikuwa ni Mengi.
Akiongozwa na Wakili Ngalo, Mengi alidai Manji alimkashifu, kumchafulia jina na kumdhalilisha kupitia matangazo aliyoyatoa kwenye magazeti yanayochapishwa nchini kwa lugha ya Kiswahili.
Magazeti hayo, ambayo aliyataja na kuyatoa mahakamani hapo kama kielelezo ni pamoja na Tanzania Daima, Mtanzania, TazamaTanzania na Majira.
Mengi alidai Manji alimwita mwongo, mzushi na kwamba, amezoea kuzusha uongo kwamba, anatishiwa maisha na kwamba, yeyote aliyemzushia uongo amekuwa akikamatwa. Alidai kauli hizo zimemchafulia jina lake na kumuathiri kisaikolijia.
Wakili Ngalo alimuhoji Mengi iwapo ana tabia ya uongo na aliwahi kuitwa polisi kuhusiana na madai hayo ya Manji.
Mengi alijibu kuwa hajawahi kuitwa polisi wala kusema uongo kama ilivyodaiwa na Manji, badala yake amekuwa akisaidia watu mbalimbali, wakiwamo watu wenye ulemavu, pia ni mwanamazingira na amekuwa akipambana na ufisadi.