Mfumo wa teknolojia ya ufuatiliaji wa magari yaliyoibwa unaojulikana kama Cartrack umeonyesha mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake.
Ofisa Mauzo wa Kampuni ya CarTrack, Fredrick Magadi, aliliambia gazeti hili kuwa mfumo huo umekuwa unawaepusha watu mbali mbali pamoja na taasisi binafsi na za umma dhidi ya hasara inayoweza kutokea kutokana na kuibwa kwa vyombo hivyo.
 Alisema mfumo huo ambao hutumia teknolojia iliyounganishwa na mfumo wa GSM na satelaiti huweza kufuatilia na kuonesha sehemu gari iliyoibwa ilipo na hivyo kuwafanya wamiliki wa vyombo vya usafiri waliounganishwa na mfumo huo angalao kuwa na amani.
Kwa habari zaidi.....
 Alisema kwa kupitia mfumo huo wa Cartrack uliwezesha kukamatwa kwa gari la serikali lenye namba za usajili STK 7080 mali ya Wizara ya Ujenzi lililokuwa limeibwa Jumamosi Desemba 4, mwaka huu na kukutwa nyumbani kwa Mbunge wa zamani wa Mpanda Magharibi, Abdallah Sumry ambaye anatuhumiwa kuhusika na wizi huo.
 Akifafanua alisema kutokana na gari hilo kuwa limeunganishwa kwenye mfumo wa teknolojia unaoendeshwa na kampuni hiyo ukiwa ni mtandao wa mfumo wa mawasiliano ya simu na satelaiti (GSM).
 Aina hiyo ya mtandao ni mkubwa na wa kuaminika na unaokua kwa haraka kwenye nyanja ya mawasiliano hususani kwenye kufuatilia na kuyanasa magari yaliyoibwa na kurudishwa kwa wamiliki wake halali.
Alisema katika utendaji wa teknolojia hiyo sio tu kwamba inawezesha timu za ufuatiliaji kubaini sehemu lilipo gari bali pia inawezesha mmiliki wa gari kubaini mwenendo wa gari lake kupitia mtandao wa intaneti.
 "Mara nyingi inapotokea kwamba gari liko mikononi mwa mtu mwingine huwa tunawasiliana na mmiliki kwa simu kuulizia kwanini lake linaendeshwa na mtu mwingine” alisema.
 "Majibu tunayopata ni kwamba labda amempa mtoto wake au dereva mwingine, lakini inapokuwa kinyume chake kwamba halipo kwenye umiliki huo wa ridhaa hapo inakuwa limeibwa na kazi inayofuata ni kuhakikisha mfumo wa Cartrack unalifuatilia hadi sehemu litakapoegeshwa na kujulisha vyombo vya usalama kwa ajili ya kulikamata na kulirudisha mikononi mwa wamiliki halali."alisema
 Alisema mfumo wa CarTrack unatumia betri la gari lenyewe kama chanzo cha mawasiliano na ikitokea kwamba umeme unaoingia kwenye betri hiyo umefunguliwa huonekana na hivyo kushindwa kufanya kazi kwake hufuatiliwa hadi kupatikana kwa gari lenyewe.