Mbunge wa Jimbo la Mtama katika wilaya na mkoa wa Lindi, Benard Membe amewataka madiwani wa halmashauri ya Lindi vijijini kuacha tabia ya usiri na majungu badala yake wajenge utamaduni wa kushikamana ikiwemo kusimamia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.
Membe aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza katika kikao cha kwanza cha madiwani hao kilichoenda sanjari na kumchagua mwenyekiti wa halmashauri hiyo, kilichofanyika mjini hapa, juzi.
Akizungumza na madiwani hao, Membe ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa kimataifa, alisema baadhi ya halmashauri hapa nchini zinakosa maendeleo kutokana na madiwani wake kuendekeza majungu na usiri.
Waziri huyo alisema kutokana na tabia hiyo, mara nyingi kunasababisha migongano mingi isiyo ya msingi kati yao, viongozi na watendaji, badala ya kusimamia na kudhibiti vema matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo.
Alisema imekuwa ni kitu cha kawaida kuona na kusikia baadhi ya halmashauri zetu kuwepo kwa miradi isiyo kamilika kwa wakati wala kutekelezwa, licha ya mabaraza ya madiwani kuridhia miradi hiyo itekelezwe.
Mbunge huyo, alisema hali hiyo inachangia kwa madiwani kutokuwa na umoja, mshikamano, umakini katika kuhoji, kusimamia na kufuatilia mwenendo wa uendeshaji wa miradi ya maendeleo ya wilaya au ya jimbo.
Waziri Membe alisema ili miradi iweze kukamilika kwa wakati na kutoa mafanikio yanayotarajiwa kwa wananchi, madiwani kwa ushirikiano na wataalamu wanapaswa kutekeleza majukumu yao, kwa kuzingatia misingi mizuri ya sheria, taaluma na uadilifu.
Membe amewataka pia madiwani kuwa wabunifu wa vyanzo vipya vya mapato na kupunguza, matumizi yasiyo na tija, ili kuipunguzia halmashauri utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.
Alisema kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na wananchi katika kuwachagua madiwani wapya pamoja na kumpata mwenyekiti mpya wa kuongoza halmashauri hiyo ya Lindi Vijijini, anatarajia kuona mabadiliko makubwa ya maendeleo yakipatikana ili jamii iendelee kuwa na imani na CCM.
Katika uchaguzi huo, madiwani wamemchagua aliyekuwa Katibu Tarafa ya Lindi mjini, kabla ya kuwa Manispaa, Methew Makwinya kuwa mwenyekiti mpya wa halmashauri, baada ya kumdondosha aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kwa miaka kumi, Ahamadi Mbonde.