Mahabusu 20 kati ya 28 kutoka Gereza la Keko jijini Dar es Salaam, jana waligoma kushuka kwenye gari ili kuingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kusikiliza kesi zao.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2:30 asubuhi katika viunga vya mahakama hiyo ambapo mahabusu wanane waliteremka kwenda kusikiliza kesi zao huku wengine 20 wanaodaiwa kukabiliwa na kesi za mauaji kugoma kuteremka wakidai kutaka kuonana na Waziri wa Katiba na Sheria.
Wakiwa ndani ya basi lenye namba za usajili STK 5829 linalomilikiwa na Jeshi la Magereza, mahabusu hao walisikika wakisema wameamua kugoma kuingia mahakamani kutokana na kesi zao za unyang’anyi wa kutumia silaha na za mauaji kucheleweshwa kukamilika upelelezi.
“Sisi hatuteremki tunataka haki itendeke kila siku tukiletwa hapa mahakamani kesi zetu upelelezi bado haujakamilika na wenzetu wengine hapa shahidi mmoja anakuja kila baada ya miezi sita. Tunasota mahabusu miaka mitano bila kujua hatma yetu,” walisikika wakisema kwa nyakati tofauti bila utaratibu.
Hata hivyo, baada ya juhudi za kuwasihi mahabusu hao kushindikana, saa 4:00 asubuhi gari hilo liliondoka eneo la mahakama na kuwarejesha mahabusu.
Akizungumza ofisini kwake, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kwey Rusema, alisema mahabusu wanane waliokubali kuteremka kesi zao zilisikilizwa jana.
Mapema wiki iliyopita, washtakiwa wanaokabiliwa na kesi mbalimbali zilizopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, walifanya mgomo kama huo kutokana na madai yanayofanana na kulazimika kurudishwa mahabusu.