POLISI mkoani Rukwa wamewakamata watu 30 wanaosadikiwa kuwa majambazi.

Watu hao wanakabiliwa na tuhuma za unyang'anyi na uvunjaji wa nyumba mjini Sumbawanga.

Watu hao pia wanatuhumiwa kuwavamia wakazi wa mjini hapa nyakati za usiku katika baa na maeneo ya starehe na kuwanyang'anya mali zao na fedha taslimu.

Kwa siku za karibuni mjini hapa kulijitokeza wimbi la vijana waliokuwa wakiwavizia watu usiku na kuwajeruhi kwa nondo na mapanga na kuwanyang'anya mali zao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Isuto Mantage amesema leo kuwa, kundi la vijana hao wakiwa na silaha za jadi, wamekuwa wakivamia baa na kuwajeruhi wanywaji na kuwapora mali zao.

Katika matukio mbalimbali ya ujambazi yaliyowahusisha watuhumiwa hao, zaidi ya Sh 800,000 na simu za viganjani zenye thamani ya zaidi ya Sh 500,000 na mali yenye thamani ya mamilioni ya shilingi viliporwa.

Kamanda Mantage amesema, kutokana na hali hiyo, Polisi imefanya msako maalumu na kukamata watuhumiwa zaidi ya 30 na wengi wao walitambuliwa na kwenye magwaride ya utambulisho na watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

"Katika msako huo, zilikamatwa mali mbalimbali ambazo baadhi yake zimetambuliwa na wenyewe kwamba ziliibwa kwenye matukio mbalimbali ya unyang'anyi na uvunjanji,” alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, bado kuna mali zingine zinasubiri kutambuliwa na wenyewe.