Ufisadi wa ardhi umedhihirika mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alipotembelea maeneo ya wazi yaliyovamiwa huku majina makubwa yakitajwa kuhusika, mojawapo la waziri wa zamani, Joseph Mungai.
Akitoa maelezo jana mbele ya Waziri Tibaijuka, Mkurugenzi wa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Albina Burra, alisema kuwa kiwanja namba 586 na 587 kitalu F kilichopo eneo la Msasani Village kilivamiwa na mmiliki mmoja ambaye alimtaja kwa jina la Shia Ithnasheri.
Alisema kuwa mmiliki huyo alikuwa akifuatilia kupatiwa hati miliki kwa muda mrefu na kwamba alishindwa kuipata kutokana na kiwanja hicho kuwa mali ya umma.
Burra alisema mmiliki huyo baada ya kukosa hati hiyo, aliamua kukiuza kwa Mungai ambaye aliwahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne. Mungai alitoka serikalini Februari 2008.
Alisema kuwa taratibu za kubadilisha matumizi kutoka eneo la wazi kuwa makazi hazikufuatwa, hivyo Mungai kukosa kibali cha ujenzi katika manispaa kutokana na tatizo hilo.
Alisema Mungai aliendelea kutafuta hati miliki ya eneo hilo ambapo ilishindikana na kujulishwa kuwa eneo hilo alipatiwa kinyemela na kwamba ni mali ya umma.  jana tulimtafuta Mungai kwa ajili ya kupata ufufanuzi, lakini simu zake mbili za kiganjani zilikuwa zimefungwa. Maeneo mengine ambayo Waziri Tibaijuka aliamuru majengo yaliyojengwa yabomolewe haraka jijini Dar es Salaam ni kiwanja namba 59 kilichopo eneo la Ocean Road jirani na Hospitali ya Aga Khan na kingine ni kiwanja namba 1006 kilichopo eneo la Palm Beach.
Profesa Tibaijuka alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifanya ziara ya kuzungukia katika maeneo ambayo yameachwa wazi kwa ajili ya matumizi ya umma ili kuwabaini wavamizi wake.
Viongozi wengine waliokuwa katika ziara hiyo ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Ubungo, John Mnyika; Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugalile; Mkurugenzi wa Wilaya ya Kinondoni, Raphael Ndunguru; Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Leonidas Gama, na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Chiku Gallawa.
Profesa Tibaijuka aliagiza majengo katika viwanja hivyo yabomolewe haraka hata kama wamiliki hao wamefungua kesi mahakamani.
“Hata kama wamefungua kesi nimesema kuwa mahakama haiwezi ikazuia zoezi la ubomoaji na mahakama pia haiwezi ikamruhusu kuendelea na ujenzi katika eneo hilo wakati inajulikana wazi kuwa eneo hilo ni la matumizi ya umma na sio katika matumizi mengine,” alisema.
Burra alisema kuwa kiwanja cha Ocean Road kilijengwa kinyemela na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mwaka 2002 aliingilia kati kwa kutoa amri kwamba kiwanja cha Palm Beach kisitumike kwa matumizi mengine binafsi kwa kuwa ni mali ya umma.
Burra alisema kuwa wamiliki wa eneo la wazi la Palm Beach, S.N Patel na G.N Patel waliamua kujenga eneo hilo kwa nguvu kwa madai kuwa mahakama imewaruhusu. Alisema kuwa kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa mahakamani na iliandika barua kwa Wizara ya ya Ardhi kutaka kiwanja hicho kigawanywe ili mmiliki huyo apatiwe eneo. Burra alisema kuwa alishindwa kusaini barua hiyo kwa kuwa eneo hilo halitakiwi kutumiwa katika matumizi binafsi.
Alisema baada hapo mahakama iliwatumia barua nyingine ikiwahoji sababu za kutojibu barua ya kwanza. Aidha, Burra alisema kuwa wizara haikujibu.
Profesa Tibaijuka alisema kuwa kitendo hicho cha mahakama kutaka kiwanja hicho kiwaganywe inaonyesha dhahiri ni rushwa ilitembea.
Alisema kuwa kama Rais Mkapa alishatoa amri kuwa kiwanja hicho ni mali ya umma inawezekanaje tena mahakama kutaka kigawanywe.
Hata hivyo, Waziri Tibaijuka alisema kuwa viwanja vyote vinatolewa kwa mujibu wa ramani na sio kwa njia za kinyemela.
“Ramani inaonyesha wazi kuwa hilo eneo ni mali ya umma na litaendelea kuwa hivyo ingawa kuna nyumba amejifanya kuijenga kwa haraka haraka atabomoa haraka,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Tibaijuka alizungukia maeneo mengine ambayo pia yamevamiwa na baadhi ya vigogo.
Maeneo mengine ambayo yameuzwa kinyemela na kushuhudiwa na Tibaijuka ni kiwanja namba 1072 kilichoko Upanga, Oysterbay Beach, eneo la viwanja namba 1272, 1273, 1274, 1275 vilivyopo barabara ya Kaole, kiwanja namba 615 Msasani na Msasani Bonde la Mpunga kiwanja TP 1/618/888.
Tibaijuka pia alitembelea bonde la Msimbazi na Hananasif Kinondoni na kujionea wananchi wanavyoishi mabondeni na kusema wananchi hao wanatakiwa kuboreshewa makazi yao.
“Unajua hawa wanachokitaka sio kiwanja kwani kuna wengine walishapatiwa viwanja na matokeo yake kuviuza na kurudi kuishi katika mabonde hayo,” alisema Waziri Tibaijuka.
Alisema kuwa wananchi hao wanataka kuishi maeneo ya karibu na mji kutokana na kufanya kazi maeneo hayo au biashara zao zipo karibu.
Alisema Wizara yake itashirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha kwamba wataboresha nyumba au kujenga mpya ili wananchi hao wahamishiwe huko. Tibaijuka alisema kuwa waliovamia maeneo hayo wavunje haraka majengo kufikia mwisho wa mwezi huu wasipofanya hivyo litaletwa tingatinga kufanya zoezi hilo.
Hata hivyo, alitoa pole kwa wale waliouziwa viwanja kinyemala.
Tibaijuka alisema kuwa amejipanga upya katika kuboresha jiji la Dar es Salaam ili liwe na makazi endelevu.
Kwa upande wake, Mnyika alimpongeza Tibaijuka kwa kuanza kushughulikia uvamizi wa maeneo ya wazi, lakini akamtaka apitie na kuifanyia kazi ripoti kuhusu uvamizi wa maeneo ya wazi jijini Dar es Salaam.