Baadhi ya vigogo wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoani Kilimanjaro wanadaiwa kutumia vibaya mtandao wa malipo ujulikanao kama Pre-Arrival Declaration (PAD SYSTEM) kwa kutoza kodi kwa masilahi binafsi na kusahau uchumi wa nchi.
Katika juhudi za TRA kukuza ufanisi wa kazi zake walifikia uamuzi wa kuanzisha mfumo wa kuwa na kituo kimoja (centralized) wa ukadiriaji kwa kuwaweka maofisa wake wote wa ukadiriaji wa kodi katika vituo vyote vya forodha katika chumba kimoja Jijini Dar es Salaam ili kutoa makadirio ya kodi kupitia mtandao huo. habari zaidi gonga hapoo chini...
Kuna juhudi za kuhujumu mpango huo kutokana na baadhi ya maofisa wa TRA kuwakwamisha wateja kwa madai kwamba mtandao uko chini, hali inayotoa mwanya wa kubembelezana kwa nia ya kupata chochote.
Maafisa hao wanadaiwa kutoza gari aina ya Mitsubishi Fuso Sh 100,000 hadi Sh 500,000 kwa njia ya mawakala wao (vishoka) ili kupangiwa bei upesi na kwa wateja wanaoonekana kutokukubaliana na mawakala hao magari yao huendelea kushikiliwa na TRA bila kupewa bei za kulipia kwa madai kuwa mtandao ni mbovu kwa siku kadhaa.
Hali hiyo imesababisha magari zaidi ya 1,000 kurundikana katika yadi ya TRA Holili huku wateja wake wakiendelea kulala katika nyumba za wageni wakisubiri TRA iwaruhusu kulipia kodi magari yao kutoka Dubai na Japan.
Kufuatia hali hiyo, kampuni za uwakala wa Mizigo katika mpaka wa Holili, KIA na Tarakea wanakusudia kugoma ilikushinikiza wateja wao wahudumiwe na TRA bila ya kuwepo urasimu na mazingira ya rushwa.
Mawakala hao wamedai kuwa bei ya lori la Fuso ushuru wake unajulikana ni Sh milioni 6 wakati Toyota Corolla chakavu ni Sh million 2.7 wakati mpya ni Sh milioni 1.8
" Tumeshawaandikia TRA tufanye kikao nao tuwaeleze kuwa kwa hali hii wanaihujumu nchi … haiwezekani mtu anunue gari likae mwezi mmoja hapa Holili na mizigo yake wakati bei zinajulikana,”alilalamika mmoja wa mawakala aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini
Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Patiecia Minga na Kamishna wa Forodha nchini, Waridi Kaburu waliliambia NIPASHE kwa nyakati tofauti jana kuwa wamesikitishwa na taarifa hizo na kuwa watachunguza madai hayo ya wateja.
Minga alisema kuwa amewasiliana na Meneja wa TRA Holili kujua ni sababu gani zimepelekea mrundikano wa magari katika kituo hicho.
Kaburu alisema amemuagiza Minga kufuatilia suala hilo na kumpatia taarifa haraka kwa kuwa haamini kuwa kituo kidogo kama cha Holili kinaweza kuwa na mrundikano wa magari zaidi ya 1,000.
" Niko mbali na ofisi kwa sasa, lakini nitamuagiza RM Kilimanjaro afuatilia na mimi pia nitafuatilia,” alisema Kamishna Kaburu.
Mtandao huo ulianzishwa baada ya mtandao wa awali wa TISCAN kulalamikiwa na wadau wa TRA.
Uchunguzi umeonyesha kuwa urasimu huo wa TRA umeongeza wateja wa kupitia njia za panya mkoani Kilimanjaro ambao unakadiriwa kuwa na njia zaidi ya 450 kwenda Kenya.