Notisi ya saa 48 ya kuondoka kwenye eneo linalomilikiwa na Kampuni ya Image Properties and Estates, imetolewa kwa Yusuf Manji na Afisa Mtendaji Mkuu wa makampuni matano yaliyopanga kwenye eneo la kampuni hiyo.
Notisi hiyo ilitolewa Desemba 20, mwaka huu kupitia barua yenye kumbukumbu namba DLA/IMAGE/2010/12.
Ilitoka kwenye kampuni ya Uwakili ya Destiny Law Attorneys ya jijini Dar es Salaam kwenda kwa Afisa Mtendaji wa makampuni hayo ikilekeza aione Manji.
Makampuni yaliyotajwa katika barua hiyo iliyosainiwa na Wakili Benitho Mandele, ni Quality Group Limited, Gaming Management Limited, Quality Logistics Co. Limited, International Transit Investment Limited na Q- Consult Limited.
Barua inamtaarifu Manji kwamba, imepewa maelekezo na mteja wao, Kampuni ya Image Properties and Estates na inamtaarifu ifuatavyo:-
“Wewe ni mpangaji ndani ya jengo la Quality Plaza Complex lililo katika Plot namba 189/2, bararaba ya Nyerere mali ya PSPF. Kwamba kuanzaia Aprili 11, 2009 mpaka Desemba 2010 una limbikizo la deni linalofikia Dola za Marekani 2,335,189,06”, ilieleza.
Iliongeza: “Kiasi hicho hakijumuishi dola 1,197,456,09 unazodaiwa katika Shauri la Ardhi Namba 33 la Mwaka 2009 ambalo bado liko mahakamani.”
Aidha, barua hiyo inasema: “Ulishindwa kulipa kiasi hicho cha pesa bila sababu yoyote ya msingi, kwamba kushindwa kwako kulipa deni hilo kunaathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za mteja wetu na mmiliki PSPF. Mbali na hilo, umepewa notisi nyingi za kuachia eneo ulilopanga, lakini hukuitikia wito huo.”
Ikamalizia kwa kumueleza kwamba anapewa saa 48 ya kuondoka katika maeneo aliyopanga ndani ya jengo hilo, vinginevyo hatua kali dhidi yake zitachukuliwa baada ya muda huo kupita.
Mbali na notisi hiyo, Manji alifahamishwa pia kuwa gharama za kumuondoa katika maeneo aliyopanga katika jengo atazibeba yeye.