Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, ametoa msaada wa nyungo mbili za kukamata vituo mbalimbali vya runinga katika Gereza la Musoma kwa lengo la kuwasaidia wafungwa kupata habari na taarifa mbalimbali za nchini na ulimwengu kwa ujumla.
Vincent alitoa msaada huo jana na kuukabidhi kwa Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Mara, Abel Chitama, mjini hapa.
Alisema wakati akijinadi, aliahidi kuboresha mazingira ya wafungwa ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia wanapata haki za kibinadamu ikiwemo kupata habari na mazingira bora ya afya.
kwa habari zaidi....
Alisema nia na madhumuni yake ya kutoa msaada huo kwa wafungwa ni kuwasaidia kupata habari ambazo zitawapa elimu na njia ambazo wanatakiwa kuzifuata katika kutafuta haki zao na walio mahabusu kupata elimu ambayo itawaonyesha njia ya kufuatilia ili kesi zao zisikilizwe ipasavyo.
“Wafungwa na mahubusu wengi hapa nchini hawaelewi haki zao kutokana na kutopata habari za kuwaelimisha, hivyo watatumia nyungo hizi katika kupata elimu kutoka vituo mablimbali vya runinga,” alisema.
Vincent alisema mfungwa anaruhusiwa kupata habari hata kama yuko kifungoni na kwamba kufungwa si chanzo cha kupoteza uelewa wa dunia.
Aidha, alisema anakusudia kufufua michezo kwa maaskari magereza kwa jinsia zote mbili, mpira kwa askari wa kiume na kike pamoja na michezo mingi iliyokuwa ikichezwa na maskari hao kwa kuwapatia vifaa vya michezo pamoja na kuwafadhili katika mashindano.
Naye Afisa Magereza huyo Chitama alitoa shukrani na kusema kuwa wafungwa watanufaika na nyungo hizo katika kupata habari za ulimwengu na mafunzo mengine.