Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (Chadema), imeitaka serikali kulaani hadharani matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya kidemokrasia ya kimataifa unaofanywa na Laurent Gbagbo na wafuasi wake nchini Ivory Coast.
Aidha, kurugenzi hiyo inatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kutamka hadharani kumtambua, Alassane Ouattara kuwa ndiye mshindi wa kiti cha urais katika nchi hiyo na kulaani vitendo vinavyofanywa na Gbagbo na wafuasi wake.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa Chadema, John Mnyika ilisema.
“Inashangaza kwamba wakati Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na serikali za nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika zimetoa matamko ya wazi serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya diplomasia ya kimya.
Hii ni tofauti kabisa na wakati wa Mwalimu Nyerere ambapo Tanzania ilikuwa mstari wa mbele na kutoa misimamo ya wazi ya kukemea vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora”.
Chadema imesema inatambua kwamba Rais Kikwete alizungumzia kidogo matatizo ya Ivory Coast wakati akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Amani katika eneo la Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika hivi karibuni nchini Zambia.
Katika mkutano huo Rais Kikwete alieleza kwamba suala la Ivory Coast linashughulikiwa na mikono salama na akaonyesha matumaini yake kwamba pande mbili zenye mgogoro zitafikia makubaliano.
“Kauli hii ya Rais Kikwete inalea vitendo vya ukiukwaji wa misingi ya demokrasia vinavyofanywa na Laurent Gbagbo na wafuasi wake kwa kuwa inatoa fursa kwa mgombea ambaye taasisi zote huru zimetamka kuwa ameshindwa katika uchaguzi kuanza majadiliano na aliyeshinda badala ya kumpisha katika uongozi wa nchi”.
Ni muhimu serikali ya Tanzania ikaeleza msimamo wake kwa uwazi ili kuondoa mashaka kwamba ukimya wake unatokana na Rais Kikwete kukosa uhalali wa kimaadili (moral authority) wa kukemea vitendo vya ukiukwaji wa demokrasia na mchakato wa uchaguzi uliomuingiza madarakani kuhojiwa kutokana na tuhuma za matokeo ‘kuchakachuliwa’ katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Chadema imesema inapinga kauli ya Rais Kikwete kuwa mgogoro wa Ivory Coast uko katika mikono salama wakati ambapo kumefanyika mauaji ya raia wasio na hatia siku chache zilizopita na sasa wanajeshi wanaomuunga mkono Gbagbo wamewazingira wafuasi wa Ouattara katika Hotel Golf katika jiji la Abijan na kukwaza shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) ndani ya nchi hiyo.
“ Serikali ya Tanzania inapaswa kufanya kazi kwa niaba ya wananchi, na msimamo wa raia wa Tanzania unafahamika bayana kwamba wengi hawakubaliani na viongozi kuingia madarakani wa chaguzi zisizo huru na haki.
Tunatarajia kwamba kama hali ya mambo itaendelea kuwa tete nchini humo, serikali ya Tanzania itaungana na wapenda demokrasia wengine wanaotoa mwito kwa Gbagbo kuwekewa vikwazo mbalimbali”.