Katibu wa Uenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), John Chiligati, ameelezea kukerwa kwake na wanasiasa anaodai walikuwa wakimchafua katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 31, mwaka huu na kuzifananisha siasa zao na za majitaka.
Aidha, amesema hatagombea ubunge mwaka 2015 kwa sababu atakuwa na umri mkubwa wa miaka 65.
Alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kuchagua Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni uliofanyika kwenye ofisi za CCM wilayani hapa.
Chiligati ambaye pia ni Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), alisema wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, kulijitokeza maneno mengi dhidi yake kutoka kwa wapinzani wake ambayo alidai hayakuwa na ukweli wowote zaidi ya kumchafua ili wananchi wasimpe kura.
"Naomba tushikamane, ziko dalili tulizoanza kuziona wakati ule wa kura za maoni, siasa za majitaka za kuchafuanachafuana majina, tumeanza kuziona wakati ule. Oh sijui Chiligati hatakiwi, sijui kazomewa, sijui wapi maneno ya ajabu kabisa mimi sitakiwi kwa lipi? " Alihoji.
Aliongeza: "Hata wakati wa kura za maoni, bado kura zinahesabiwa wameshapeleka Chiligati ameshaanguka, kagaragazwa, wingi wa maneno lakini maneno yale yakiendekezwa ndiyo yanayojenga chuki, uhasama na mifarakano."
Chiligati aliwahakikishia wapinzani wake kwamba yote hayo yalijitokeza kutokana na kutaka kura za kuchaguliwa kuwa wabunge wa jimbo hilo, lakini kwa bahati nzuri yeye ameyaacha, ameyasamehe na hana habari tena na watu waliokuwa wakimchafua katika kipindi hicho.
"Wengine sisi majina yetu tumejenga sifa miaka mingi sana sasa mtu anapokuchafua na hayo magazeti yanasomwa nchi nzima na wengine wanakupigia simu hivi imetokea nini? Unaweza kukasirika na kuacha kumsalimia mtu wa aina hiyo," alisema.
Aliwashauri madiwani hao baada ya kukabidhiwa dhamana ya kuwaongoza wananchi wa Manyoni wawe makini kusimamia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo na kuweka mbele maslahi ya waliowachagua.
" Sasa jamani kwa wale mnaotaka nafasi hii hivi sasa mimi nimefikia umri wa kustaafu, nina miaka 60 na kwa mwaka 2015 nitakuwa na miaka 65. Inatosha kabisa napumzika na nataka niache Manyoni uongozi mmoja, wilaya moja na maendeleo yanaonekana," alisisitiza.
Aliwataka madiwani hao kusimamia shughuli za maendeleo kwa kuzingatia haki, sheria na wajibu wa matumizi ya fedha za serikali bila kuwaonea watendaji na kujiepusha kununuliwa na watendaji hao kwa lengo la kuwahujumu wananchi wao.