Kampuni ya Benchmark Production kupitia kwa mkurugenzi wake Rita Poulsen, jana ilikabidhi zawadi kwa mshindi wa shindano la nne, Mariam Mohamed pamoja na washiriki wote walioingia 5-bora ya shindano la Bongo Star Search 2010.
Makabidhiano ya zawadi hizo yalifanyikia kwenye jengo lililokuwa la BSS House Mikocheni jijini Dar es salaam mbele ya waandishi wa habari.
Mariam alikabidhiwa zawadi yake ya kuwa mshindi wa kwanza ya Sh. milioni 30 kutoka kwa wadhamini, Kampuni ya Bia (TBL) na pia Sh. milioni moja kutoka Mariedo Boutigue.
James Martin alikabidhiwa Sh. milioni 10 kwa kushika nafasi ya pili na Joseph Payne alipewa Sh. milioni 5 baada ya kushika nafasi ya tatu.
Bella Kombo aliyeshika nafasi ya nne alipewa Sh. milioni moja na Waziri Salum aliyeshika nafasi ya tano, pia alipewa Sh. milioni moja.
Ruth Oscar alizawadiwa Sh. milioni moja kwa kuwa mshiriki mwenye nidhamu.
Mara baada ya kukabidhi zawadi hizo, Rita alisema licha ya wao kuwasaidia wasanii hao, lakini juhudi binafsi za washindi hao ndizo zitakazowasaidia zaidi katika kuendeleza vipaji vyao.
Fainali za shindano hilo zilifanyika Ijumaa kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.