MCHEZAJI mmoja wa ridhaa atakayebahatika atacheza na Tiger Woods kwenye michuano ya pro am (wachezaji wa kulipwa na wa ridhaa) ambayo itafanyika kabla ya Dubai Desert Classic Februari mwakani.

Woods, ambaye atarejea kwenye michuano ya European Tour baada ya kuwa nje miaka miwili amekubali kucheza pro am, lakini wachezaji wa ridhaa wana nafasi ya kukutana na mchezaji anayeshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ubora duniani Woods.
Kutokana na utaratibu wa Dubai, ambao mtu anaweza kujiandikisha bila malipo kwenye mtandao mchezaji yeyote anaweza kupata nafasi ya kucheza na Woods na hivyo wachezaji wa ridhaa wa Tanzania pia wana nafasi ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Kila mchezaji duniani ambaye ana handicap (kiwango cha ubora) inayotambulika anaweza kujiandikisha kupitia mtandao wa www.golfindubai.org na mshindi atapatikana wiki mbili kabla ya michuano itakayofanyika kwenye viwanja vya gofu vya Emirate Dunai kwa mujibu wa taarifa kutoka Dubai.

Kwa upande wa wanaume wanaotakiwa kujiandikisha ni wenye handicap 18 na kushuka wakati kwa wanawake ni kuanzia handicap 26 kushuka.

Lengo la michuano hiyo ni kuinua gofu Dubai kupitia wachezaji nyota kama Woods baada ya kunakosa msisimko.

"Lengo la kutengeneza ratiba kupitia mtandao ni kuhamasisha wachezaji wa ridhaa kushiriki," alisema Mohamed Juma Buamaim, makamu mwenyekiti na mtendaji mkuu wa kampuni ya gofu Dubai ambayo inaandaa michuano.

"Kucheza na Tiger ni ndoto ya kila mmoja," alisema. "Nina hakika mchezaji mwenye bahati wa kiume au wa kike atajifunza baadhi ya vitu kwa kumuangalia wakati wa kucheza karibu."

Woods alishinda taji la Desert Classic mwaka 2006 na 2008 na hajawahi kushika chini ya nafasi ya tano tangu mwaka 2001.

Mwaka 2009 alikosa michuano kutokana na kusumbuliwa na goti na mwaka huu alikosa kutokana na kashfa iliyofunika maisha yake binafsi.