Mfungwa aliyehukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha, ameuweka katika wakati mgumu uongozi wa Magereza Mkoa wa Shinyanga, baada ya kukutwa na jinsia zote mbili na zote zikifanya kazi kama kawaida.
Mfungwa huyo alikuwa katika Gereza la Malya lililoko wilayani Maswa baada ya kuhukumiwa, hali iliyosababisha mkanganyiko kwa uongozi huo kuhusu sehemu ambayo anapaswa kuwekwa gerezani.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Magereza mkoani hapa, Elika Pesha, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkasa huo.
Kwa habari zaidi....
Hata hivyo, ofisa huyo alikataa katakata kutaja jina la mfungwa huyo kwa madai kuwa kufanya hivyo ni sawa na kumdhalilisha.
Alisema baada ya uongozi wa gereza kuona utata huo, uliamua kumpeleka mfungwa huyo hospitali ya Bugando jijini Mwanza kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu ndipo iligundulika kuwa jinsia zote zinafanya kazi.
Pesha alisema kuwa tayari taratibu za kumpeleka Muhimbili jijini Dar es Salaam kufanyiwa upasuaji baada ya kupata ushauri kutoka kwa madaktari zimekamilika na kwamba mfungwa huyo atapatiwa fursa ya kuchagua ni jinsia gani iondolewe.
Alisema katika upasuaji huo kitakachozingatiwa zaidi ni ushauri wa wataalamu, ambao wengi wanaona kuwa ni bora abaki na jinsia ya kiume kwa sababu umbile lake linaonyesha kuwa ni mwanaume.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Mkoa wa Shinyanga, Issa Magori, aliyesikiliza kesi ya mfungwa huyo na kuitolea hukumu alisema mwaka 2007, mfungwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga kwa kosa la unyanganyi wa kutumia silaha akiwa na wenzake watatu.
Alisema walivamia kwenye ofisi ya biashara ya almasi na kuiba mzani wa kupimia madini hayo, simu mbili pamoja na mashine ya utambuzi wa almasi.
Hakimu Magori alisema mfungwa huyo pamoja na wenzake walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na walipokaguliwa kabla ya kupelekwa gerezani ndipo walipogundua kuwa mmoja wa wafungwa hao anajinsia mbili na zote zinafanya kazi.
“Mfungwa huyo hana maziwa, isipokuwa ana ndevu sauti yake ni ya kiume na jina lake ni la kiume kwa ujumla muonekano wake ni wa jinsia ya kiume kutokana na hali hiyo uongozi wa magereza umeamua kumuweka chumba maalumu chini ya uangalizi mkubwa,” alisema.
Alieleza kuwa tangu aanze kazi hiyo hajawahi kutoa hukumu kwa mtu ambaye ana jinsia mbili na zote zinafanya kazi na kwamba tukio kama hilo lilishawahi kutokea mkoani Kagera kwa mtu ambaye alikuwa ana jinsia mbili, lakini kati ya hizo moja ndiyo ilikuwa ikifanya kazi.