Rais wa Fifa Sepp Blatter, ametania kwamba mashabiki wa soka ambao ni mashoga watakaokwenda kwenye Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, hawana budi "kujizuia kufanya mambo yao ya ngono."
Makundi ya kutetea haki za mashoga, wameshutumu uamuzi wa kupeleka mashindano hayo ya Kombe la Dunia katika nchi ambayo ushoga ni marufuku.
Lakini Blatter, akatania kwa kusema: "Ningependa kusema, mashabiki wa soka walio mashoga, wajizuie na mambo yao watakapokuwa Qatar."
Na katika taarifa ambayo ni kali zaidi, Blatter amesema: "Nina hakika wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia yatakapofanyika Qatar, hakutakuwa na matatizo."
Hata hivyo mchezaji nyota wa zamani wa NBA John Amaechi, ambaye alijitangaza rasmi kuwa shoga mwaka 2007, ameshutumu vikali kauli hiyo ya Blatter.
Qatar ambayo ni nchi ya Kiislamu, ilipata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2022, wakizishinda Australia, Japan, Korea Kusini n Marekani, wakati wajumbe wa kamati ya utendaji ya Fifa walipopiga kura tarehe 2 mwezi huu wa Desemba.

Tangu wakati huo Fifa imekuwa ikishutumiwa kutokana na uamuzi wao wa kupeleka mashindano hayo kwa mara ya kwanza eneo la Mashariki ya Kati.
Wasiwasi umeibuka kuhusu kuandaa mashindano hayo wakati wa miezi ya kiangazi katika nchi ambayo joto linakuwa la kiwango cha juu cha nyuzi joto 40 vipimo vya centrigrade hadi nyuzijoto 50, huku sheria ikikataza unywaji wa pombe hadharani.
Makundi ya kutetea haki za mashoga na mashoga wenyewe, pia wameonesha wasiwasi wao kuhusiana na kuruhusiwa watu wanaoendekeza vitendo hiyo wanaopenda soka, kwenda Qatar na wamelaani uamuzi wa Fifa na wametangaza kususia shughuli zote zinazohusiana na Kombe la Dunia mwaka 2022.