Zaidi ya Sh. milioni 7.5 zilizokuwa zikipelekwa Benki ya Biashara (NBC), Tawi la Moshi zimeokolewa baada ya mfanyakazi wa kampuni ya kuuza vinywaji ya Machare Investiment, Caroline Ibrahimu aliyekuwa akipeleka fedha hizo benki kumng'ang'ania mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi aliyetaka kupora fedha hizo.
Habari kutoka ndani ya jeshi la polisi ambazo hazijathibitishwa zinasema polisi wa doria wa pikipiki (jina lake halikutajwa) ndiye alichora ramani kwa kushirikiana na jambazi huyo kwa kukodisha pikipiki kutoka katika moja ya gereji mjini hapo na kwenda kuiegesha karibu na benki hiyo kumsubiri Caroline.
Chanzo hicho cha habari kinabainisha kuwa tukio hilo lililojiri majira ya saa 5 za asubuhi jana, zinadai kuwa Caroline baada ya kufika benki alipaki gari na kutoka na fedha hizo ndipo alipovamiwa na jambazi huyo na kumkwapua fedha hizo jambo lililomfanya amng'ang'anie jambazi huyo kwa kumshika kiunoni huku akiburuzwa chini kuelekea ilikopaki pikipiki.
Baadhi ya mashuhuda walioshuhudia tukio hilo, walisema mara baada ya msichana huyo kuendelea kumng'angania jambazi huyo ambaye hakuwa na silaha, baadhi ya madereva taksi waliokuwepo jirani walijitokeza kutoa msaada na ndipo dereva aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo kutaka kuondoka huku msichana huyo akiwa bado amemshika jambazi huyo kiunoni na kuendelea kuburuzwa chini.
Shuhuda huyo Peter Michael alisema mara baada ya dereva wa pikipiki kuzidiwa nguvu aliibwaga pikipiki kwenye mtaro wa maji machafu.
Hata hivyo, fedha zote zilifanikiwa kuokolewa baada ya msichana huyo kutumia ujasiri wa kumng'ang'ania jambazi huyo.
Muda mfupi baadaye polisi walifika na kumkuta jambazi huyo akipigwa na wananchi lakini walimuokoa kwa kuondoka naye pamoja na msichana huyo kuelekea katika kituo cha polisi.
"Kwa kweli huyu mwanamke ni komandoo, pamoja na kuporwa fedha hizo lakini alimng'ang'ania jambazi hilo kufa na kupona hadi pesa zake akazipata...ila cha kushangaza ni polisi aliyekuwa zamu hapo benki, hakujishughulisha baada ya kuona mwanamke huyo ameporwa, japo kuwa alikuwa na bunduki, sasa jamani usalama wa jeshi la polisi upo wapi?" Alihoji Peter kwa masikitiko.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lucas Ng'hoboko, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alikiri kutokea na kusema kuwa yeye yupo mkoani Arusha lakini taarifa kamili atazitoa mara baada ya kurudi mkoani kilimanjaro.