Viongozi duniani wameonesha kumuunga mkono mgombea wa upinzani wa urais nchini Ivory Coast Alassane Ouattara, wakisema yeye ndio mshindi halali wa raundi ya pili ya uchaguzi wa urais.
Baraza la Katiba la nchi hiyo limepindua matokeo, na kumtangaza Rais Laurent Gbagbo mshindi, na anatarajiwa kuapishwa rasmi muda mfupi ujao.
Marekani, Umoja wa Mataifa, Ufaransa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, Ecowas, zimemtaka Bw Gbagbo kukubali kukubali matokeo ya kushindwa.
Uchaguzi huo ulikuwa na nia ya kuiunganisha nchi hiyo baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002.
Waziri Mkuu Guillaume Soro wameonya kuwa kubadili matokeo ya uchaguzi kunatishia jitihada za kuleta amani na kuiunganisha nchi hiyo.
Siku ya Alhamisi, Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) ilitangaza kuwa Bw Ouattara ameshinda uchaguzi wa Novemba 28 wa raundi ya pili, kwa asilimia 54.1, dhidi ya 45.0 ya mpinzani wake.
Lakini baada ya Bw Gbagbo na wafuasi wake kutuhumu kuwa kuna wizi wa kura, Baraza la Katiba likatengua matokeo hayo.
Mwenyekiti wa baraza hilo Paul Yao N'Dre amesema Bw Gbagbo amepata asilimia 51 ya kura.
Shirika la habari la serikali ya Ivory Coast limesema Bw Gbagbo ataapishwa Jumamosi.