RAIA sita wa kigeni wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kwa tuhuma za kukutwa na kete 31 za dawa ya kulevya zenye thamani ya Sh milioni 930.

Mwendesha Mashitaka Daniel Buma aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Diaka Brama (52) raia wa Guinea, Ndijano Abubakar (50) raia wa Liberia, Sylvia Namrembe (34) wa Uganda, Farida Kiswule (26) wa Uganda, Robson Teise (32) wa Uganda na Ismail Mugabi (40) pia wa Uganda.
Mbele ya Hakimu Ester Mwakalinga, Buma alidai kuwa washitakiwa hao walikamatwa Juni 23, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Buma alidai mahakamani hapo kuwa baada ya kupekuliwa kwenye mabegi yao, washitakiwa hao walikutwa na kete hizo za kokeni zenye thamani ya Sh milioni 930, walizokuwa wakisafirisha kutoka Brazil kuja Tanzania kwa ajili ya kuuza.

Alidai kuwa washitakiwa hao walikutwa na hati za kusafiria zinazowatambulisha kuwa wao ni mabalozi na ni wafanyakazi katika Ubalozi wa Guinea.

Hata hivyo, Wakili Steven Urasa alidai kesi ya wateja wake ni ya kubambikiwa kwani walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Killimanjaro (KIA) na sio Julius Nyerere, kama upande wa mashitaka unavyodai.

Washitakiwa walikana shitaka na walirudishwa rumande hadi upelelezi utakapokamilika na Januari 5, mwakani kesi yao itatajwa tena.

Katika hatua nyingine, watu wawili wamepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo ya Ilala kwa tuhuma za wizi wa fedha.

Washitakiwa ni Veila Adamu (25) na Gabriel Njoka, wote wakazi wa Kinondoni. Mbele ya Hakimu Tarsila Kisoka, Mwendesha Mashitaka Aida Kisumo, alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Julai 10 na Oktoba 31, mwaka huu katika eneo la Ukonga Banana.

Kisumo alidai washitakiwa waliiba fedha taslimu Sh milioni 18 kwa kutumia mashine ya ATM yenye namba 67090100205146183 kutoka benki yenye namba 61512770001, mali ya Eliachia Malisa.

Washitakiwa walikana shitaka na walirudishwa rumande hadi Januari 7, mwakani kesi
itakapotajwa tena.