Rais wa zamani wa Afrika Kusini amewasili nchini Ivory Coast kuwakilisha Umoja wa Afrika kusaidia kusuluhisha mzozo wa kisiasa.
Laurent Gbagbo na mgombea wa upinzani Alassane Ouattara wote wamekula kiapo cha kuongza nchi, baada ya kudai kupata ushindi katika raundi ya pili ya uchaguzi.
Awali Bw Ouattara alitangazwa mshindi, lakini matokeo hao yalitenguliwa na kupewa Bw Gbagbo anayetetea kiti chake.
Umoja wa Afrika umeonya kuwa mzozo huo unaweza kuleta "matatizo makubwa".
Katika taarifa iliyotolewa, umoja huo umezitaka "pande hizo mbili kuonesha uvumilivu na kujizuia kuchukua hatua ambazo zitaleta matatizo katika hali ambayo ni tete".
Nchi kadhaa na mashirika ya kimataifa - ikiwemo marekani, Umoja wa Mataifa Ufaransa na Shirika la Fedha Duniani IMF - zimeunga mkono kutangazwa kwa Bw Ouattara kuwa mshindi wa kura hiyo iliyopigwa Jumapili iliyopita.