Serikali ya Zanzibar imetoa karipio kwa viongozi wa serikali wanaokiuka taratibu za ugawaji wa ardhi.
Serikali imesema kuwa vitendo hivyo vinafanywa na viongozi kwa kutumia nyadhifa zao kwa lengo la kudhulumu ardhi ya wananchi.
Akizungumza na wakazi wa Kitope, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema Serikali imepata taarifa juu ya baadhi ya viongozi kutenga kwa ajili ya viwanja vya michezo na maeneo ya wazi ardhi ya wananchi bila ridhaa yao. na kwa habari zaidi...
“Wananchi wananyang’anywa ovyo ardhi na kutengwa kuwa viwanja vya michezo na maeneo ya wazi, bila idhini ya wamiliki,” alisema Balozi Iddi.
Balozi Iddi alikuwa anazungumza katika mkutano wake na viongozi wa ngazi ya wilaya na masheha wakati akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kushiriki kikamilifu kufanikisha Uchaguzi Mkuu uliopita katika Jimbo la Kitope.
Akionekana kukerwa na tabia hiyo, Balozi Iddi aliagiza viongozi waliohusika katika vitendo hivyo kufuta nyaraka walizotoa baada ya kugawa ardhi na maeneo hayo.
Alisema pamoja na kufuta nyaraka walizotoa kwa ajili ya kuhalalisha umiliki mpya wa maeneo hayo, viongozi hao pia wawarejeshee mara moja waliotoa fedha kununulia maeneo hayo.
“Watendaji wa ngazi zote zilizohusika kugawa ardhi hiyo kinyume cha taratibu, wakiwemo masheha, watendaji wa Halmashauri waache mara moja tabia hiyo na kurejesha fedha walizouzia maeneo na kufuta mara moja nyaraka walizozitoa,” alisema Balozi Iddi.
Balozi Iddi alisema iwapo agizo lake halitatekelezwa, Serikali haitasita kuchukua hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwatimua kazi viongozi wote waliotuhumiwa katika kashfa hiyo.
Alisema kuondolewa kazini kwa watendaji hao hakutakwamisha juhudi ya Serikali kuwatumikia wananchi.
Serikali itaendelea kuwatumikia wananchi kwa manufaa yao, badala ya kulinda watumishi wanaofanya kazi kwa maslahi binfasi, alisema.
Balozi Iddi alisema pamoja na kupambana na vitendo vya ukiukaji wa sheria na taratibu za utendaji, Serikali pia imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuwaondolea wananchi kero katika maeneo mbali mbali, Pemba na Unguja.