Juzi, timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimajanro Stars’ ilifanya kile ambacho Watanzania wote walikuwa wakikisubiri baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Burundi na kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.habari zaidi....
Ni matokeo muhimu yaliyoihakikishia Stars nafasi ya kuendelea kusaka ubingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya 34 tangu ianzishwe mwaka 1974, huku pia yakiipa nafasi Zanzibar kutinga pia robo fainali kwani yaliiacha Burundi yenye pointi nne kama Zanzibar kuzidiwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa na kupoteza nafasi ya kuwemo miongoni mwa timu mbili zilizomaliza katika nafasi ya tatu huku zikiwa na matokeo bora kwenye makundi yao.
Sisi tunaona kuwa baada ya Stars kushinda juzi, sasa nafasi ya kulibakisha kombe la Chalenji iko wazi kwa Stars na ndugu zao Zanzibar na zipo sababu kadhaa za kuamini hivyo.
Maelfu ya mashabiki waliofika uwanjani juzi kiasi cha kuujaza uwanja unaochukua watu 60,000 na wengine kulazimishwa kuondoka uwanjani hapo kwa mabomu ya machozi na pia gari la maji ya kuwasha la polisi, ni dalili kwamba Stars wana uhakika wa kupata uungwaji mkono mkubwa, hivyo ni juu yao kucheza vyema kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho wakati watakapocheza dhidi ya Rwanda keshokutwa Jumatano.
Mabadiliko ya kikosi aliyofanya kocha Mdenmark wa Stars, Jan Poulsen, yaliisaidia timu hiyo kucheza kwa kujituma zaidi kulinganisha na mechi zao mbili za awali dhidi ya Zambia na hata ile waliyoshinda 3-0 dhidi ya Somalia.
Tunaamini kuwa, kama Stars itaonyesha tena kandanda safi na kujituma kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho wakati watakapocheza dhidi ya Rwanda, ni wazi kwamba watashinda na kutinga robo fainali na kuendelea na michuano hiyo itakayofikia tamati Jumapili.
Hali kama hiyo iko pia kwa ndugu zao Zanzibar, ambao walionyesha kucheza kwa kujituma tangu mechi yao ya utangulizi waliyoshinda dhidi ya Sudan na hata walipofungwa na Ivory Coast na kutoka sare na Rwanda.
Hata hivyo, tunadhani kwamba kuna umuhimu wa kuwakumbusha wachezaji wa Stars na Zanzibar watakaocheza dhidi ya Uganda kuwa, kamwe wasilewe sifa wanazopata sasa baada ya kufika robo fainali.
Badala yake, waendelee kujituma mazoezini ili wasifanye makosa keshokutwa, kwani Watanzania wataendelea kujaa kwa wingi kwenye Uwanja wa Taifa ili kuwashangilia na kwa sababu hiyo, haitakuwa vizuri kuwaangusha.
Jambo la muhimu ni kuongeza umakini katika safu zao za ushambuliaji, hasa katika kikosi cha Stars ambacho wachezaji wake wanasifika kwa kukosa magoli ya wazi.
Mabeki wa timu zote wanapaswa kujiimarisha pia na kocha kutoka England, Hall Stewart wa Zanzibar, kama ilivyo kwa mwenzake Poulsen, wanatakiwa kuhakikisha kuwa makosa ya kujipanga vibaya kwa mabeki wao kama ilivyoonekana katika mechi za hatua ya makundi yanamalizwa.
Kamwe hatutarajii kuziona Stars na Zanzibar zikiwaangusha Watanzania kwa kutobeba kombe kama walivyofanya wakati Bara walipokuwa wenyeji pia wa michuano ya miaka ya 1981, 1992, 2002 na 2007.
Nyota wa Stars na Zanzibar wana kila sababu ya kuitumia fursa waliyo nayo sasa na hatimaye kubakisha Kombe la Chalenji nchini kama ilivyokuwa mwaka 1974. Kila la kheri Kilimanjaro Stars, kila la kheri Zanzibar Heros.