MTANDAO wa Wikileaks umeendelea kufichua taarifa zinazotokana na nyaraka za siri, na safari hii imeitaja Tanzania kuwa moja ya nchi kumi zinazotumiwa zaidi kama kituo cha kupitishia dawa za kulevya barani Afrika.

Nchi jirani ya Kenya, nayo imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zilizopo katika orodha hiyo ya nchi zinazotumika kama njia ya kupitishia dawa hizo haramu.

Madai hayo yamekuja siku chache baada ya mtandao wa Wikileaks kuibua mambo mazito juu ya Tanzania, moja likidai Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea anakwamishwa na Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua katika kesi muhimu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Hosea alitoa maelezo hayo juu ya mustakabali wa mapambano dhidi ya ufisadi nchini na ugumu uliopo katika kuwashtaki watuhumiwa wa ufisadi mkubwa. Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa na Dk. Hosea mwenyewe.

Aidha, mtandao huo umedai kufichua siri nyingine nzito kuwa Tanzania ni kitovu cha usafirishaji wa madini ya uranium kwenda Iran.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na mtandao huo Januari 2006 Balozi William Bellamy aliwahi kuwashutumu polisi kwa kuficha ushahidi uliokuwa katika faili la Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuhusu taarifa za mwaka 2004 za dawa za kulevya aina ya kokeni zenye thamani ya Sh bilioni 6.

Taarifa zaidi zinadai kuwa Bara la Afrika limekuwa njia kuu ya biashara ya kokeni zinazokamatwa Uholanzi ambazo zinasadikiwa kusafirishwa kwa meli kutoka Kenya.

Tayari Serikali ya Uholanzi imeshawakamata watu wengi wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo mtoto wa mbunge wa zamani wa Kenya.

Taarifa za mtandao huo kutoka Maputo, Msumbiji zinadai kuwa nchi hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la biashara za kulevya baada ya kutumika kama kituo kikuu cha kusafirisha dawa za kulevya zinazopelekwa katika nchi za Afrika Mashariki.

“Biashara ya dawa za kulevya ni tatizo linaloota mizizi Msumbiji kwa kuwa biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya zinazosafirishwa kwa usafiri wa anga na wa majini kutokea Asia ya Kusini na Amerika Kusini,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Inadaiwa kuwa, usimamizi duni wa sheria na rushwa ni mambo yanayochochea wasafirishaji wa dawa za kulevya kupita katika nchi za Afrika kwa uhuru.

Taarifa ya mtandao huo inasema kuwa Jiji la Maputo Msumbiji limekuwa njia kuu ya wasafirishaji dawa za kulevya aina ya kokeni ambao husafiri kwa ndege kutoka Brazil kupitia miji ya Johannesburg Afrika Kusini, Lisbon Ureno au Luanda, Angola.

Kuna mitandao miwili ya kusafirisha dawa za kulevya ambayo inafanya kazi Msumbiji na Kusini Mashariki mwa Asia.

Katika nchi ya Mali, ndege ambayo haikutambuliwa ilianguka katika jangwa Novemba 2009 na inasadikiwa ilikuwa imebeba kokeni kutoka Marekani ya Kusini.

Ndege hiyo aina ya Boeing 727-200 ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 10 za dawa za kulevya. Taarifa zilizotolewa na Mtandao wa Marekani zinaonesha kuwa vielelezo vinavyothibitisha kuwapo kwa biashara za dawa za kulevya katika nchi jirani na nchi zinazotajwa kuwa vinara wa biashara hiyo barani Afrika.

Taarifa za mtandao huo zinaonesha jinsi Ghana ilivyoshindwa kuonesha vielelezo kuhusu mashua iliyoingia nchini humo mwaka 2007 ikitokea Marekani ya Kusini. Iliachiwa na kuendelea na safari zake bila hata ya uchunguzi wa kina.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Ghana mwaka 2009, Rais wa Ghana, John Atta Mills, aliwashuku viongozi waliokuwa kwenye msafara wake wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya kupitia njia anayopita Rais katika Uwanja wa Ndege wa Kotoko jijini Accra na kuomba maofisa waandamizi wa uhamiaji wa Uingereza kufanya upekuzi ili kuepuka kero inayotokana na kushukiwa kuwa wamebeba dawa za kulevya.

Januari mwaka huu Rais Mills alimwambia Katibu Msaidizi wa Barack Obama kuhusu masuala ya Afrika, Johnnie Carson kwamba anahofia juu ya maisha ya baadaye ya watu wa Ghana, ilipomtafuta kwa simu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba ili azungumzie madai hayo, alipopokea simu hakuwa tayari kuzungumzia madai hayo badala yake akashauri gazeti hili kuwasiliana na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso.

Hata hivyo, simu ya msemaji huyo haikupatikana.