Ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo unatarajiwa kuanza mwaka 2012, uamuzi ambao umechukuliwa kupunguza mlundikano wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.Akiwasilisha mada katika Kongamano la Kimataifa la Bandari la Afrika na Ulaya, linaloendelea jijini hapa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Julius Mfuko, alisema upembuzi yakinifu tayari umekamilika.kwa habari zaidi...
Alisema wazo la kujenga bandari hiyo katika mji wa kihistoria wa Bagamoyo utarahisisha uondoaji wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo yamekuwa yakirundikana na hivyo kuwa moja ya tatizo kubwa ambalo bandari hiyo imekuwa ikikabiliana nalo kwa miaka sasa.
Mfuko alisema ujenzi huo unaotarajiwa kuanza 2012 unatarajiwa kukamilika mwaka 2013.
Hata hivyo, Bandari ya Bagamoyo itahudumia Ukanda wa Kiuchumi wa Biashara (EPZ).
Alisema kati ya hatua nyingi za muda mrefu za kutafuta ufumbuzi wa tatizo la mrundikano wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam, TPA inatarajia kuanzisha bandari mpya na kubwa za nchi kavu (ICD) wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani.
“Tuna mpango wa kujenga bandari kubwa ya nchi kavu kule Kisarawe, ambako mizigo yote itakayokuwa ikisafirishwa na reli itakuwa ikitumia bandari hiyo,” alisema.
Kisarawe ipo kilomita 25 kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, na gharama ya upembuzi yakinifu ina gharimiwa na Benki ya Dunia (WB).