MAELFU ya wapenzi wa muziki wa dansi na Injili juzi walijitokeza kuuaga na kuuzika mwili wa aliyekuwa mwanamuziki mahiri Ramadhani Mungamba Mtoro ‘Dk. Remmy’.

Mwili wake uliagwa viwanja vya Biafra Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Emanuel Nchimbi, Mbunge wa Ubungo John Mnyika, Mbunge wa Kinondoni Iddi Azan pamoja na wanamuziki wa dansi, injili, taarabu na wadau wengine wa muziki pia walikuwepo.
Akitoa salamu za serikali, Waziri Nchimbi alisema mchango wa Dk. Remmy hautosahaulika kutokana na aina ya ujumbe aliokuwa akiimba na kuwa ulienda na wakati na masuala mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza.

Alisema atakumbukwa kwa mchango wake katika masuala mbalimbali muhimu kama vile kuhamasisha vita dhidi ya umasikini, magonjwa na kuzungumzia masuala ya kijamii.

Kauli hiyo pia ilizungumzwa na mwimbaji wa Injili, ambaye amepata kuimba na Dk. Remmy kwenye muziki wa dansi Cosmas Chidumule, ambaye pia aliwataka wanamuziki kuiga mfano wa Dk. Remmy kutunga nyimbo zenye ujumbe.

Alisema Dk. Remmy hakuwa na majivuno kama wasanii wengine wa sasa ambao husahau majukumu yao katika jamii na kuanza kuimba nyimbo zisizofaa.

“ Sio wanamuziki wa nyimbo za kisasa au za dansi tu, ila hata wanamuziki wa Injili nao wanatakiwa kujifunza kitu kutoka kwa Remmy, hakuwa na majivuno hakuwa na muda wa kupoteza kazini aliheshimu wapenzi wa muziki wake,” alisema Chidumule.

Naye Askofu wa Kanisa la Pentekoste, David Mwasoko alimmwagia sifa marehemu kuwa alikuwa mwanamuziki mwenye wito na kipaji cha ajabu katika muziki aliyekitumia kipaji chake kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Alisema Remmy aliamua kukata rasta zake ili kutumia muda wake kumtukuza Mungu kitendo ambacho ni baraka kubwa kwa msanii huyo.

Wanamuziki wa Injili walikuwapo katika viwanja hivyo, waliimba nyimbo kadhaa za dini, huku wengine wakiimba nyimbo za zamani za Remmy za kidini na za kiulimwengu.

Mwili wa marehemu uliagwa na wapenzi wengi wa muziki ambapo kulikuwa na misururu mirefu kutoa heshima hiyo na kisha wengi walijitokeza kwenye maziko alasiri katika makaburi ya Sinza, Dar es Salaam.