Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England (FA) Roger Burden ameondoa jina lake kuwania nafasi ya kudumu ya Uenyekiti, baada ya England kukosa nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018.
Burden, ambaye aliteuliwa mwezi wa Mei, amesema hawezi kuwaamini tena wajumbe wa kamati ya utendaji ya Fifa, baada ya England kuikosa nafasi hiyo na badala yake kwenda Urusi.
Amesema: "Natambua sehemu muhimu ya majukumu yangu ni kuwa karibu na Fifa, ambalo ndio Shirikisho linalosimamia mchezo wa soka duniani."
"Siko tayari kufanya kazi na watu ambao siwaamini na nimejiondoa kuwania nafasi ya uenyekiti wa kudumu," aliongeza Burden mwenye umri wa miaka 64.
Maafisa wa kamati ya England ya kutafuta nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 wamesema wajumbe sita kati ya 22 wa Fifa waliahidi kuipigia kura England.
Lakini hatimaye England iliambulia kura mbili tu, moja kutoka kwa Muingereza, Geoff Thompson - hali iliyoihakikishia kutoka mapema katika kinyag'anyiro hicho, wakati wa kupiga kura mjini Zurich siku ya Alhamisi.
Ameongeza kueleza mwenyekiti huyo anayestaafu: "Tuna uhuru wa vyombo vya habari katika nchi yetu na sote hatuna budi kuishi na kuafiki mawazo yoyote yanayotolewa kulingana na wakati."
"Lakini hakuna shaka yoyote soka la Uingereza linanufaika sana na namna vyombo vya habari vinavyoitangaza na vingetoa nafasi kubwa ya kwa mashindano ya Kombe la Dunia kama yangepata nafasi ya kuandaliwa England.
"Sina ugomvi na Urusi kupata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia. Nina hakika wataandaa vizuri mashindano hayo na nimewapongeza."
Lakini Kaimu Mwenyekiti huyo wa FA bado ameshindwa kufumbua fumbo la kwa nini England ikaambulia kura mbili tu.