Akizungumza kabla ya maandamano yaliyopangwa na wafuasi wa mmoja wa wagombea wawili wanaodai kushinda uchaguzi nchini Ivory Coast, katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon meonya kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi na kupelekea kuzuka kwa machafuko makubwa nchini humo.
Wafuasi wa bwana Alassane Ouattara wanasema baadaye leo Alhamisi watajaribu kukiteka kituo cha Televisheni ya kitaifa; na kusisitiza kuwa maandamano yao yatakuwa ni ya amani.
Jeshi ambalo linathibitiwa na mpinzani wa bwana Outtara; rais wa sasa Laurent Gbagbo limewashutumu waandamanaji hao kwa kuchochea makabiliano kimakusudi. Ban Ki Moon ametaka pande zote mbili kujiepusha na vitendo vyovyote vitakavyoleta vurugu.
Bwana Ouattara anaaminika na wengi kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo hivi maajuzi na bwana Ban amekariri wito wake wa kumtaka bwana Gbagbo ajiondoe madarakani.