Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti anadhani timu yake ilicheza kwa kuogopa katika kipindi cha pili walipotoka sare ya bao 1-1 na Everton siku ya Jumamosi.habari zaidi....
Chelsea imeweza kupata pointi tano katika mechi sita zilizopita za Ligi Kuu ya England na hawajaweza kushinda michezo minne iliyopita.
"Tulianza kuogopa wakati Everton walipokuwa wakilisakama lango letu," alisema Ancelotti, ambaye timu yake hivi sasa inakabiliwa na mechi dhidi ya Tottenham, Manchester United na Arsenal.
"Kipindi hiki ni kigumu, lakini hatupo mbali na kilele na hatuna sababu ya kuwa na wasiwasi kama ilivyotokea kipindi cha pili."
Mabingwa hao watetezi walianza kwa kishindo katika mechi tano za mwanzo za msimu wa Ligi Kuu ya England, wakifunga mabao 21 katika mchakato huo, lakini kiwango hicho kimepotea na sasa kujikuta nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi.
Akizungumzia mechi dhidi ya Everton Ancelotti alisema: "Kipindi cha pili hatukudhibiti mchezo kabisa - tulipoteza nidhamu yetu na nusura washinde mchezo ule kutokana na mashambulizi yao ya kushtukiza.
"Nina wasiwasi ndiyo, kwa sababu hatushindi mechi. Kipindi cha pili tulishindwa kabisa. Hatukucheza kabisa mchezo wetu."
Chelsea mara ya mwisho kushinda ilikuwa tarehe 10 mwezi wa Novemba ilipoilaza Fulham - na tangu wakati huo wakapoteza mchezo dhidi ya Sunderland na Birmingham na kwenda sare walipocheza na Newcastle na Everton.