Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameendeleza moto wake na safari hii amewajia juu wanaopokea rushwa katika vituo vya mizani na kusema dawa yao inakuja.
Waziri Magufuli amesema katika kuwadhibiti wala rushwa hao, serikali itaboresha vituo vya mizani ya kupimia uzito wa magari kwa kuweka mitambo ya kamera ili kuwanasa wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na wizi wa fedha za umma katika vituo hivyo.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, wakiwemo wa Tanroads, wakala wa ufundi na umeme na nyumba mkoani Kilimanjaro.
Dk. Magufuli alisema mitambo ya kamera itakayofungwa itayafuatilia magari yote yanayopita katika vituo hivyo kwa kuwa yapo baadhi ya makampuni ya magari yanayoshirikiana na Tanroads kukwepa kulipa faini wanazopaswa kulipa kutokana na kuzidisha uzito wa mizigo katika magari yao.
Alisema katika Mkoa wa Mwanza, watumishi wa Tanroads wanatuhumiwa kwa upokeaji wa rushwa kutokana na magari yanayozidisha uzito, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa barabara na hivyo kuilazimu serikali kutumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya matengenezo.
Alisema amepokea malalamiko mengi juu ya ulaji rushwa katika vituo vya mizani na kuwaonya wanaojihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa kwa magari yanayozidisha uzito kuacha mara moja.
Alisema hatapenda kuona wafanyakazi wanakamatwa kwa rushwa kwani wanamtia aibu yeye pamoja na serikali, hivyo hatavumilia kuona vitendo hivyo vikifanyika.
Waziri huyo alisema haiwezekani kusikia kituo kinakusanya Sh. milioni 36 kwa mwezi, lakini matumizi yake ni Sh. milioni 30.
Alisema kuanzia sasa hakuna vibali vya kusamehe magari yanayozidisha uzito vitakavyotolewa na badala yake maofisa wa mawakala wa barabara wasing’ng’anie kukaa maofisini pekee na badala yake watembelee vituo vya mizani na kuwanasa wafanyakazi wala rushwa.
Dk. Magufuli pia alisema serikali kamwe haitasita kuwachukulia hatua kali mkandarasi wanaotengeneza barabara chini ya viwango kutokana na kuwekeana mikataba ya ulaji na watumishi wa Tanroads na kutoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutoa taarifa za mkandarasi feki.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, mwaka huu, serikali imetenga Sh. bilioni 177, lakini inaonyesha kuwa fedha nyingi zitatumika katika masuala ya utawala badala ya matengenezo ya barabara.