WATU sita wa Kijiji cha Nongwe, katika Wilaya mpya ya Gairo, Mkoa wa Morogoro wanashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kuwashambulia askari Polisi kwa mawe na mapanga na baadaye kuharibu gari la Jeshi la Polisi kwa kuvunja vioo na vitu  mbalimbali
vilivyokuwa ndani yake.

Tukio hilo limeelezwa kutokea wakati wanausalama hao walipokuwa kwenye operesheni maalumu ya kuwasaka wezi wa pikipiki. habari zaidi....
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Shaaban Kimea, amethibitisha kwa kusema kuwa, polisi hao walikuwa kwenye msako wa wizi wa pikipiki kimkoa ulioanza tangu Julai, mwaka huu.

Katika kipindi hicho, matukio 103 ya wizi wa pikipiki yameripotiwa, lakini ni 21 tu ndizo zilizopatikana.

Kutokana na tukio la juzi, Kamanda huyo aliwataja wanakijiji wanaoshikiliwa kwa kuwapiga polisi na kuharibu gari la jeshi hilo kuwa ni Justine Yohana (22), Pancras Ally (14), Noel Lazaro (18) na Ibrahim Ngunga (23) wote wakazi wa Kijiji cha Nongwa.

Kaimu Kamanda huyo pia aliwataja askari wa upelelezi waliojeruhiwa kuwa ni Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi, Benedict Nyamagatala ambaye alikuwa kiongozi, Sajenti Lukuba, Konstebo Sajingwa ambaye ni dereva wa gari la Polisi, Konstebo Anorld na Koplo Idd.

Alilitaja gari la Polisi lililoharibiwa vibaya na watuhumiwa hao kuwa ni lenye namba za
usajili PT 1997 aina ya Toyota Land Cruiser.

Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu mashitaka
yanayowakabili.

Akizungumzia mkasa huo kwa kina alisema Desemba 2 mwaka huu, saa 3 asubuhi mjini Morogoro, askari walifanikiwa kumkamata Sebastian Chanile ( 29) mkazi wa Dakawa ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kutokana na kuhusika na uhalifu.

Alisema baada ya kukamatwa alihojiwa na kukiri kuhusika na wizi wa pikipiki na alimtaja mwenzake Maheza Muhehe (29) kuwa ndiye amekuwa akishirikiana naye katika wizi wa pikipiki hizo walizokuwa wanaziuza katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro.

Alisema baada ya Muheza kukamatwa alihojiwa naye alikiri kuiba pikipiki na kutoa ushirikiano kwa polisi na kutaja sehemu mbalimbali alipouza pikipiki katika eneo la Nongwa Gairo.

Alisema Desemba 4, mwaka huu, saa 6 usiku askari wa upelelezi Mkoa wa Morogoro, kwa kushirikiana na Kituo cha Gairo walianza kufanya msako wa mtandao wa wizi wa pikipiki na walianzia katika Kata ya Dakawa wilayani Mvomero.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda huyo, Desemba 6, mwaka huu, saa 6 usiku wakiwa na mtuhumiwa Maheza aliyekuwa akiwaelekeza sehemu alizouza pikipiki walifika katika Kijiji cha Nongwa na kufanikiwa kuzipata pikipiki tatu na kuwashikilia watu watatu kwa wizi huo.

Kaimu Kamanda huyo alisema, wakati askari wakiendelea kuoneshwa na Maheza maeneo aliyouza pikipiki, baadhi ya wanakijiji walitaka kuwakomboa watu waliokamatwa kwa kutumia nguvu lakini askari walifanikiwa kuondoka na kuendelea na na kazi hiyo.

Hata hivyo alisema, taarifa zilizolifikia Jeshi hilo zilidai kuwa wananchi hao waliamshana na kula njama za kuliteka gari la Polisi, baada ya kumalizika kwa msako wa pikipiki wakati walipokuwa wakiondoka kijijini hapo.

Alisema walipofika kilometa nane, askari hao walikutana na kundi la watu na kulipita lakini mita chache mbele gari lilianza kutitia kwenye mchanga na askari walipoteremka kwa ajili ya kuangalia tatizo, ghafla walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 200, ambao waliwaweka
polisi chini ya ulinzi na kuanza kuwashambulia.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda huyo, watu hao waliokuwa na mapanga, mishale, mashoka
na mawe, walikuwa wakidai kuwa askari hao ni majambazi.

Alisema mmoja wa askari alifanikiwa kutoa taarifa kwa njia ya simu katika Kituo cha Polisi cha Gairo na muda mfupi baadaye askari wa Upelelezi Mkoa, na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika katika eneo hilo na wanakijiji hao walianza kukimbia, kabla ya baadhi yao kukamatwa wao na pikipiki hizo.