Janga la kuenea kwa kasi zaidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi katika Manispaa ya Shinyanga ni kubwa hasa kwa wanawake kutokana na kundi hilo kuwa na uelewa mdogo ukilinganishwa na wanaume.
Taarifa kutoka Idara ya Afya kitengo kinacho jishughulisha na mapambano dhidi ya Ukimwi katika Manispaa ya Shinyanga zimeeleza kuwa kuwepo kwa uelewa mdogo katika kundi hilo kuna changia kuendelea kwa kasi zaidi ya maambuzi mapya ndani ya manispaa hiyo ikiwemo vijijini.
Baadhi ya akina dada na wasichana hata wale wa mashuleni wamekuwa wakijishughulisha na biashara za ngono katika maeneo kadhaa ya starehe katika mji wa Shinyanga na maeneo yaliyochangamka kwa biashara na kufanya bishara ya ‘uchangudoa”.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali kupambana na ugonjwa huo kwa kutoa elimu kwa wananchi hadi vijijini kundi hilo limekuwa na mwamko mdogo huku kiwango cha maambukizi kikiwa kwa asilimia 7.4.
Imeelezwa kuwa baadhi ya akina dada wamelichukulia suala la kuzagaa mitaani kuwa ni sehemu ya ajira kwao huku wakiendekeza ngono zisizo salama na kuongezeka kwa maambukizo mapya licha ya elimu juu ya VVU/Ukimwi kuwa imeeleweka takribani maeneo mengi nchini na hata baadhi ya maeneo kasi hiyo kuanza kupungua.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo katika kipindi cha Januari hadi Oktoba 2010,,jumla ya watu 19,739 walijitokeza kupima VVU wakiwemo wanawake 9,790 ambao miongoni mwao wanawake 954 sawa na silimia 4.8 waliopimwa walikutwa na VVU.
Katika upimaji huo wanaume waliokutwa na VVU ni asilimia 3.5 hali inayoonyesha kuwa kundi la akimama likiwa liko nyuma mno kuliko wanaume.