Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Ivory Coast zimesababisha vifo vya watu 173, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, huku shinikizo la kimataifa likiendelea kumkaba Laurent Gbagbo ajiondoe madarakani.Umoja wa Mataifa pia umethibitisha kuwa mamluki wa Liberia wanasaidia majeshi ya Bw Gbagbo.
Umoja wa Mataifa na nchi nyingine kadhaa duniani zimemtambua Bw Ouattara kama rais mpya.
Tume ya haki za binaadam ya Umoja wa mataifa inakutana mjini Geneva kujadili janga hilo. Tume hiyo imesema watu 173 wameuawa wiki iliyopita na karibu 500 kukamatwa nchini Ivory Coast.
Mwandishi wa BBC Thomas Fessy mjini Abidjan anasema kuna taarifa nyingi za msako wa usiku katika makazi ya watu wanaomtii Bw Ouattara, na majeshi ya Bw Gbagbo yanazuia waandishi kwenda katika maeneohayo na ni vigumu kuthibitisha mauaji hayo.
Wafuasi wa Bw Ouattara wametaka Mahakama ya Kimataifa kuwashitaki washirika wa Bw Gbagbo kwa uhalifu wowote ambao umefanywa.
Bw Ouattara na wafuasi wake wanaishi katika hoteli mjini Abidjan, huku wakilindwa na majeshi ya kulinda usalama ya Umoja wa Mataifa wapatao 800.
Umoja wa Mataifa umesema unatazama njia za kuimarisha jeshi lake nchini Ivory Coast, katika maeneo ambayo majeshi ya Bw Gbagbo yakiwa katika hali ya mvutano mkubwa na wafuasi wa mpinzani wake, Alassane Ouattara.