MAMIA ya waombolezaji wakiongozwa na wabunge Idd Azzan na Steven Ngonyani ‘Prof. Majimarefu’ jana walishiriki kwenye maziko ya mwanamuziki Abuu Semhando kijijini kwake Kibanda, Muheza mkoani Tanga.

Semhando alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi kutokana na ajali baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kugongwa na kisha yeye kuangukia barabarani na kukanyagwa na gari iliyokuwa ikitoka upande mwingine.

Tukio hilo lilitokea eneo la Tangi Bovu, Kinondoni Dar es Salaam wakati mwanamuziki huyo alipokuwa akirejea nyumbani kutoka Africana, ambako bendi yake ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ ilikuwa ikitumbuiza.
Ilikuwa ni huzuni ya aina yake wakati mwili wa Semhando ambaye alikuwa mpiga drams mahiri, ulipowasili mapema jana asubuhi kisha kwenda kuswaliwa na baadaye kuzikwa majira ya saa nane mchana.

Prof. Majimarefu ambaye ni Mbunge wa Korogwe Vijijini alimuelezea Semhando kama mtu aliyekuwa akiipenda kazi yake na asiyekuwa na makuu.

Naye Azzan ambaye ni Mbunge wa Kinondoni, akitoa salamu za wananchi wa Kinondoni alimuelezea Semhando kwamba alikuwa kipenzi cha wengi na kwamba kifo chake ni pengo kwa fani ya muziki nchini.

Alielezea kuwa kifo cha Semhando sit u kimeshtua familia yake bali pia fani ya muziki kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki aliuelezea msiba wa Semhando kuwa si wa Twanga Pepeta pekee bali wanamuziki wote na Watanzania kwa ujumla.

“Nimefanya kazi na Semhando, imeniuma sana, alikuwa mshauri mzuri na kwa kweli wanamuziki karibu wote tulimpenda, lakini ndio dunia ilivyo,” alisema Choki akizungumza na gazeti hili juzi.

Wanamuziki mbalimbali wa bendi ya Twanga Pepeta na bendi nyingine nchini walikuwapo kwa wingi kwenye maziko hayo.

Mwanamuziki huyo aliyejiunga na Twanga Pepeta karibu miaka 12 iliyopita akitokea bendi ya Diamond Sound kwa muda mrefu ndiyo Katibu wa bendi hiyo.

Alishiriki kikamilifu katika nyimbo mbalimbali kwenye albamu karibu zote za Twanga Pepeta kuanzia Kisa cha Mpemba mwaka 1999 hadi Mwana Dar es Salaam iliyozinduliwa Juni mwaka jana.

Albamu nyingine za bendi hiyo na miaka yake katika mabano ni Jirani (2000), Fainali Uzeeni (2001), Chuki Binafsi (2002), Ukubwa Jiwe (2003), Mtu Pesa (2004), Safari (2005), Password ya Maisha (2006) na Mtaa wa Kwanza (2007).

Mwanamuziki huyo aliyezaliwa mwaka 1953 pia amepata kupigia bendi mbalimbali zikiwemo Matimila, Vijana Jazz , Orchestra Tomatoma, Safari Sound Orchestra na Tancut Almasi.