Hatimaye wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika manispaa ya Shinyanga wametoboa siri ya wagombea wa chama hicho kushindwa katika uchaguzi mkuu na kuwepo kwa mpasuko mkubwa ndani ya CCM katika jimbo la Shinyanga.
Siri hiyo imefichukuliwa na wazee wakati walipokuwa wakiwapongeza Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mbunge wa jimbo la Shinyanga, Steven Masele katika hafla fupi iliyofanyika mjini hapa na kuwashirikisha wajumbe wa baraza la wazee na wazee wakiwemo madiwani wateule.kwa maelezo zaidi...
Wazee hao wamedai kuwa sababu kubwa ya wagombea na chama hicho kupoteza viti vyao katika baadhi ya kata huku CCM ikipata kura kiduchu kwa mgombea wake wa ubunge na hata rais, walisema ni kutokana na baadhi ya wana CCM wakiwemo viongozi wa chama hicho kuisadia Chadema na hasa wagombea wake.
Mwenyekiti wa baraza la wazee wa wilaya ya kichama ya Shinyanga mjini, Alhaj Ramadhan Ibrahim alisema kumekuwepo na mpasuko mkubwa ndani CCM wakati wa uchaguzi mkuu wa jimbo la Shinyanga kwa baadhi ya viongozi wa CCM wakiwemo wajumbe wa kamati ya siasa kuhusika kukihujumu chama hicho.
Wazee hao walisema kuwa wamebaini kuwa chanzo kikubwa cha kupata ushindi mdogo na uchaguzi kuwa mgumu ni kutokana na wana CCM wenyewe kuhujumiana kwa kutoa siri za chama na hata kukisaidia Chama Cha Demkokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa hali na mali ikiwemo michago ya fedha.
Aidha, wazee hao walisema kuwa wamebaini kuwa baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wakiwemo wajumbe wa kamati ya siasa walikuwa na wanaendelea kukiunga mkono Chadema kwa kukisaidia hata fedha na katika kesi namba 5 ya 2010 iliyofunguliwa na chama hicho dhidi ya mbunge wa jimbo hilo Steven Masele wa CCM kwa lengo la kumkomoa kwa ushindi wake alioupata kuanzia kura za maoni ndani ya chama hicho.
Walisema baadhi ya viongozi hao hata katika mikutano ya kampeni ya kuwanadi wagombea wao akiwemo rais, mbunge na diwani pia hawakushiriki na badala yake walikuwa wakishiriki katika mikutano ya ndani ya CCM na kisha kutoa siri ndani ya kambi ya Chadema hali iliyosababisha CCM kukabiliwa na hali ngumu katika uchaguzi huo.
Katika maazimio ya wazee hao wamekishauri Chama Cha Mapinduzi kuchukua hatua za haraka kukisafisha kwa kutowalea wala kuwavumilia viongozi hao ambao wamepewa jina la “ndumila kuwili” na “wasaliti” na “wanafiki” wakubwa ndani ya CCM.
Aidha wazee hao wamekitaka chama hicho kuhakikisha kuwa viongozi hao wanatubu na kuomba samahani mbele ya wana CCM ili wasamehewe kwani watu hao walitarajia kuwa CCM ingeshindwa lakini sasa mambo yamekuwa kinyume kwao na ni aibu na fedheha yao.
Wakizungumzia kesi iliyofunguliwa na mgombea wa Chadema Philipo Shelembi kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Shinyanga walisema wana uhakika wa kushinda kesi hiyo endapo tu hapatakuwa na njama na hujuma toka ndani ya CCM kama zile zilizofanyika wakati wa uchaguzi mkuu.