Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo, juzi alipata wakati mgumu alipokuwa kwenye ziara yake wakati akitembelea visiwa vya Bongoyo na Mbudya baada ya boti aliyokuwa amepanda kuishiwa mafuta katikati ya bahari.
Mathayo alifuatana na waandishi wa habari kujionea hali halisi ya mazingira pamoja na kukagua utunzaji wa rasilimali za pembezoni mwa bahari.
Dk. Mathayo alipata wakati mgumu na kuanza kumuuliza dereva kama kutakuwa na madhara yoyote ambayo yatatokea baada ya boti hiyo kupoteza muelekeo na kusimama gafla.
Dereva wa boti hiyo alifanya jitihada ya kuita boti nyingine ambapo waziri pamoja na waandishi walihamia katika usafiri mwingine.
Baada ya kufika katika kisiwa cha Mbudya ambapo alimaliza ziara yake, alijukuta tena katika wakati mgumu alipokuwa akirudi katikati ya bahari wakati boti ya pili iliyobadilishwa iliisha mafuta.
“Roho yangu kwa leo imepata mshtuko wa ajabu hivi dereva tutafika kwa usalama kweli?” alihoji Dk. Mathayo.
Baada ya kumaliza ziara yake, alilitaka Jeshi la Polisi nchini kuwachukulia hatua wananchi ambao hutengeneza mabomu na kuyatumia katika kuvulia samaki hali ambayo inapelekea kuhatarisha maisha ya wananchi.