NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma na kusomewa shitaka la kumtorosha mtuhumiwa chini ya ulinzi halali wa Polisi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Emanue Mrangu Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Amon Mimata aliiambia Mahakama hiyo kwamba Zitto ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini anadaiwa kufanya kosa hilo wakati akijua jambo alilokuwa akifanya ni kosa kisheria.
Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi ASP Amoni Mimata aliieleza Mahakama Zitto alitenda kosa hilo Oktoba 27 mwaka huu, majira ya saa 5 asubuhi katika Kituo cha Polisi Mahembe katika Halmashauri Wilaya ya Kigoma.

Katika kesi hiyo namba 10 ya mwaka 2010, inadaiwa kuwa akiwa katika kituo hicho Zitto alimtorosha Peter Kibwega, mwanachama wa CHADEMA aliyekamatwa kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuhatarisha kuvunjika kwa amani.

Kwa mujibu wa mashitaka hayo Zitto anadaiwa kufanya kosa hilo kinyume cha kanuni ya adhabu kifungu cha 115 kifungu kidogo cha kwanza cha kifungu kidogo C na kifungu cha 35.

Mwendesha Mashitaka huyo wa Jeshi la Polisi alisema kuwa mtuhumiwa Kibwega anadaiwa kuhusika na vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ambapo alikamatwa na Jeshi hilo na kuanza kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo.

Wakati mtuhumiwa huyo akiwa kituoni hapo akiendelea kuhojiwa inadaiwa kuwa Zitto alifika kituoni hapo na kumchukua mtuhumiwa kwa nguvu, licha ya jitihada za polisi waliokuwapo zamu kuzuia jaribio hilo bila mafanikio.

Hata hivyo kwa upande wake Zitto amekanusha shitaka hilo na Mahakama imemwachia kwa dhamana hadi Februari 10 mwaka 2011 kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Aidha, kusogezwa mbele kwa muda mrefu kwa kesi hiyo kunafuatia ombi la Zitto Kabwe alilolitoa mahakamani hapo akiomba apate muda wa kuweza kuhudhuria vikao vya Kamati ya Bunge.