Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imesema kuwa viongozi 4,788 (sawa na asilimia 57) wakiwemo wa kisiasa na wa utumishi wa umma, hawajawasilisha matamko yao ya mali.

Taarifa hiyo ilitolewa jana jijiji Dar es Salaam katika mkutano wa waandishi wa habari na Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, wakati akitoa taarifa ya urejeshaji wa fomu za tamko la viongozi wa umma kuhusiana na rasilimali pamoja na madeni yao.
Jaji Kaganda alisema kuwa hadi sasa viongozi wa kisiasa ambao hawajawasilisha matamko yao ni 3,047 na viongozi wa utumishi wa umma ni 1,741.
Kwa mujibu wa jaji Kaganda, fomu hizo zilitolewa kwa viongozi wa kisiasa na utumishi wa umma 8,410 na kwamba waliozirejesha ni 3,770.
Jaji Kaganda alisema mwitiko huo kwa viongozi wa siasa unaweza kutafsiriwa kuwa ni mdogo kwa sababu kundi hilo linabebwa kwa kiasi kikubwa na madiwani, ambapo taratibu za uteuzi na uundwaji wa mabaraza ya halmashauri nyingi mchakato wake ulikuwa haujakamilika.
Alisema ilipofika Desemba 31, mwaka jana ni madiwani 1,032 kati ya 3,876 waliorejesha fomu za matamko ambapo asilimia 73.3 hawakuweza kurejesha.
Kuhusu viongozi wa umma, Jaji Kaganda alisema hali ya mwitiko imeathiriwa na kundi la mahakimu ambao wapo 1,631 sawa na asilimia 40.1 hawakurejesha fomu za matamko kwa wakati kutokana na hali ya jiografia ngumu na mawasiliano magumu ya nchi.
Jaji Kaganda alisema viongozi wote wa umma ambao hawakutoa tamko kwa wakati, watapewa nafasi ya kujieleza ni kwanini wasichukuliwe hatua zaidi kwa mujibu wa sheria ya maadili.
Alisema endapo maelezo yao hayataridhisha, viongozi husika wataitwa mbele ya Baraza la Maadili ambalo litawasikiliza kwa ajili ya kutoa mapendekezo kwa Kamishna wa Maadili kuhusu hatua zinazofaa kuchukuliwa dhidi ya kiongozi husika.
Baada ya hapo, Baraza litawasilisha taarifa husika kwa Rais na nakala kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya hatua mbalimbali za kiutumishi na kiutawala, alisema.
“Kazi yetu ni kusimamia kwa nguvu utekelezaji wa sheria kwa kuhakikisha kuwa mamlaka za nidhamu za viongozi husika zinawajibika ipasavyo kutekeleza mapendekezo ya sekretarieti dhidi ya viongozi wasiotekeleza misingi ya maadili,” alisema.
Kamishna huyo alisema Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imejipanga kufanya mambo mbalimbali ili kuongeza mwito wa urejeshaji wa fomu za tamko kwa mujibu wa sheria ya maadili.
Alisema kuwa jukumu lao kubwa ni kusimamia maadili ya viongozi wa umma na kuhakikisha kuwa viongozi hao wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uaminifu bila upendeleo, uonevu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
“Baraza la Maadili limeundwa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kufanya uchunguzi wa kina wa tuhuma za ukiukaji wa maadili ya viongozi,” alisema Jaji Kaganda.
Aidha, alisema viongozi hao wanatakiwa kutumia madaraka waliyokabidhiwa kwa manufaa ya wananchi na si vinginevyo.
Alisema mwaka 2005, walipokea malalamiko 78 kutoka kwa viongozi, mwaka 2006 walipokea malalamiko 222 na mwaka 2010 walipokea malalamiko 69.
Alisema kuwa malalamiko hayo yanafanyiwa uchunguzi kwa mujibu wa sheria na kwamba yatatolewa maamuzi baada ya zoezi hilo kukamilika.
Alisema maadili na utawala bora visipokuwepo katika jamii matokeo yake ni kukosekana kwa maendeleo na kuwepo rushwa.
Alisema chombo hicho ni muhimu katika juhudi za serikali katika kukuza utawala bora na misingi ya maadili nchini.
Viongozi wa kisiasa na umma walitakiwa kuwa wamewasilisha matamko kuhusu mali zao Desemba 31, mwaka jana.