Baada ya kupata mafanikio makubwa katika taarabu mwaka jana, kiongozi wa kundi la Jahazi Modern Taarab, Mzee Yussuf ametamba kuwa mwaka huu kundi lake litaendelea kuwa juu ndani na nje ya nchi kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Akizungumza  majuzi, Yussuf alisema kuwa baada ya kutamba mwaka uliopita, wamejipanga kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwa juu. Alisema kuwa siri kubwa ya mafanikio yake ni kujituma zaidi na kufanya kazi kwa bidii, jambo ambalo limewasaidia sana katika maisha yao ya kimuziki nchini.
Kundi hilo kwa sasa linatamba na kibwagizo cha ‘Juma Juma Dedee’, ambacho kimekuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa muziki wanaofika katika kumbi mbalimbali kushuhudia kundi hilo.