HATIMAYE, mama aliyejifungua watoto watano pacha hivi karibuni, Shija Maige wa kijiji cha Bulungwa wilayani hapa, amesema kutooneshwa miili ya watoto wake waliokufa ni moja ya sababu zilizomtorosha hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.

Shija alisema hayo jana alipotoa ufafanuzi katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, muda mfupi kabla ya kurudishwa Mwanza.

Alisema alilazwa wadi namba nne huku watoto wake wakiwa wadi namba mbili, kila alipotaka kunyonyesha aliitwa na wauguzi, na kila alipoitwa, alikuta idadi yao inapungua bila maelezo yoyote.
 Alisema hali hiyo ilimtisha na aliposimulia wazazi wengine wadini, walimtisha kuwa akiendelea kuwa hospitalini hapo hata yeye ‘atapelekwa machinjioni’ walikokuwa wakipelekwa wanawe hao.

Mama huyo alisema imani hiyo iliongezeka baada ya mumewe aliyemtembelea hospitalini hapo siku moja, naye kupoteza maisha.

“Sikuwa na jinsi zaidi ya kukimbia na kumwacha mtoto wangu mmoja kati ya watano aliyekuwa amebaki hospitalini,” alisema mama huyo.

Ofisa Tawala wa Wilaya ya Kahama, Paulo Cheyo, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Bahati Matala, aliagiza kwamba kutokana na mazingira yaliyoelezwa na mama huyo, vema arudishwe Bugando chini ya uangalizi wa muuguzi wa hospitali ya wilaya ya Kahama.

Mbali ya agizo hilo, alitaka pia ufafanuzi wa kina kuhusu mama huyo tangu alipokwenda hospitali ya wilaya hiyo, hadi kuhamishiwa Bugando, hali ambayo itasaidia kuweka sawa kumbukumbu za ofisi kabla ya mama huyo kwenda Bugando kujiridhisha juu ya sababu za kufariki dunia kwa wanawe hao.

Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Hellen Membe, alisema maneno ya mama huyo yanatokana na kuchanganyikiwa, baada ya kupata kifafa cha uzazi na kufariki dunia kwa watoto wake hao wanne.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Charles Majinge, alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.