Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, ametangaza itaundwa tume itakayoandika rasimu ya katiba mypa, itakayoangazia mahitaji ya nchi hiyo kwa karne ya ishirini na moja.
Katika salamu zake za mwakam mpya, Bw Kikwete amesema Tanzania inahitaji katiba itakayojali masuala mbalimbali ya kijamii na mabadiliko ya kiuchumi, kwa ajili ya kuchukua nafasi ya katiba ya sasa iliyoandikwa mwaka 1977.
Bw Kikwete amekuwa katika chagizo kubwa kutoka kwa vyama vya upinzani, tangu aliposhinda uchaguzi mkuu miezi miwili iliyopita, wakitaka iandikwe katiba mpya.
Upinzani umekuwa ukisema katiba ya sasa inakipendelea chama kinachotawala.
Mapema wiki hii, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi pamoja na maji, kuwatawanya mamia ya wapinzani waliokuwa wakiandamana katika jiji la Dar es Salaam, wakitaka mabadiliko ya katiba.